Oct 24, 2023 13:53 UTC
  • Maandamano ya kulaani jinai za Israel yafanyika Paris, Ufaransa

Maelfu kwa maelfu ya watu wamejitokeza mabarabarani katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris kushiriki maandamano ya kulaani jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina, huku idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi hadi sasa ikipindukia 5,000.

Waandamanaji hao wamekusanyika katika Medani ya Umma ya Paris kushiriki maandamano hayo ambayo ni ya kwanza kabisa kufanyika mjini hapo tangu utawala wa Kizayuni uanzishe wimbi jipya la hujuma za kutisha dhidi ya Wapalestina mnamo Oktoba 7.

Wananchi hao wa Ufaransa walioshiriki maandamano hayo wameitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua za dharura za kusimamisha mashambulizi hayo ya Wazayuni dhidi ya Wapalestina hasa wa Ukanda wa Gaza.

Waandamanaji hao walikuwa wamebeba bendera za Palestina na mabango yaliyokuwa na jumbe za kuitaka Israel isitishe mauaji ya kimbari dhidi ya wananchi wa Palestina wasio na hatia. Aidha baadhi ya mabango hayo yalikuwa na jumbe za kuunga mkono ukombozi wa taifa huru la Palestina.

Kadhalika wameilaani serikali ya Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo wakisisitiza kuwa ni mshirika wa jinai za Israel dhidi ya Wapalestina. Bango moja lina picha ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Rais wa Marekani, Joe Biden iliyoandamana na neno 'watenda jinai'.

Waandamanaji hao mjini Paris wamesema utawala katili na usiojali thamani za kiutu wa Israel umekiuka sheria zote za kimataifa, ambapo unashambulia kwa mabomu hospitali, shule na makazi ya raia wa kawaida.

Wameutaka Umoja wa Mataifa uingilie kati na kukomesha jinai zinazofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza, huku wakiitaka serikali ya Paris isimamishe misaada yake mara moja kwa utawala wa Kizayuni.

 

Tags