Belize yasimamisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i104844-belize_yasimamisha_uhusiano_wa_kidiplomasia_na_israel
Serikali ya Belize imetangaza kusimamisha uhusiano wake wa kidiplomasia na Israel kutokana na hatua ya utawala huo wa Kizayuni kukataa kusitisha vita; huku idadi ya mashahidi wa mashambulizi ya utawala huo pandikizi huko Gaza tokea Oktoba 7 hadi sasa ikikaribia watu 12,000.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 16, 2023 02:59 UTC
  • Belize yasimamisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel

Serikali ya Belize imetangaza kusimamisha uhusiano wake wa kidiplomasia na Israel kutokana na hatua ya utawala huo wa Kizayuni kukataa kusitisha vita; huku idadi ya mashahidi wa mashambulizi ya utawala huo pandikizi huko Gaza tokea Oktoba 7 hadi sasa ikikaribia watu 12,000.

Shirika la habari la IRNA jana Jumatano lilinukuu ripoti ya CNN iliyosema kuwa, Belize inalaani vikali vitendo vya jeshi la utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Taarifa ya serikali ya Belize imesema: Tumeiasa Israel itekeleza usitishaji vita haraka na iruhusu kupelekewa kwa misaada ya kibinadamu Gaza. Licha ya maombi yetu hayo, lakini Israel haijasitisha ukiukaji wa sheria za kibinadamu za kimataifa, wala kuruhusu wahudumu wa misaada ya kibinadamu kupunguza masaibu ya mamilioni wa wakazi wa Gaza.

Kadhalika taifa hilo la Amerika ya Kati limebatilisha kibali cha kuwepo balozi wa Israel nchini humo, sambamba na kusimamisha uhusiano na ushirikiano wa kidiplomasia na Tel Aviv.

Belize imejiunga na orodha ya majirani zake huko Amerika ya Latini kama Colombia, Chile, na Bolivia ambazo ama zimekata uhusiano wao na Israel au kuwarejesha nyumbani mabalozi wao kutoka Tel Aviv, kulalamikia jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Jinai za kivita za Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza

Aidha mapema mwezi huu, Afrika Kusini ilitangaza kuwarejesha nyumbani wanadiplomasia wake wote kutoka Israel, kutokana na kuendelea mashambulizi na jinai za Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Kadhalika Jumatatu ya wiki hii, wawakilishi wa bunge la Libya kwa kauli moja walipiga kura ya kujinaisha kuhusisha uhusiano na utawala wa Kizayuni, siku chache baada ya Bunge la Algeria pia kupiga kura kwa asilimia mia moja na kumruhusu Rais wa nchi hiyo kuingia vitani na utawala wa Kizayuni  kwa ajili ya kuwatetea na kuwaunga mkono wananchi wasio na hatia wa Palestina iwapo italazimu.