Jan 07, 2024 09:38 UTC
  • Umoja wa Mayahudi wa Ufaransa kwa ajili ya Amani: Israel 'inauua Uyahudi'

Umoja wa Mayahudi wa Ufaransa kwa ajili ya Amani (The French Jewish Union for Peace) UJFP umeishutumu Israel kwa "kuua Uyahudi" kutokana na mashambulizi yake ya kikatili unayofanya katika Ukanda Gaza na kueleza kwamba vyombo vya habari vya Israel vinapata burudani kwa mateso wanayopata Wapalestina.

Katika taarifa iliyotoa jana Jumamosi, UJFP imeilaani vikali serikali ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mashambulizi yake dhidi ya Gaza, ambayo imesema yameathiri pia jamii ya Israel, kwa sababu maoni ya umma ya sehemu kubwa ya jamii ya Waisrael yamejiweka mbali na ubinadamu.

Jumuiya ya Wayahudi wa Ufaransa imeashiria mashambulizi ya anga ya Israel yanayoendelea huko Gaza na kueleza kuwa Wapalestina 30,000 wameuawa au kupotea katika miezi mitatu iliyopita.

Katika taarifa yake hiyo UJFP imesema: "idadi hii, ambayo ni sawa na asilimia ya Wafaransa waliopoteza maisha katika kipindi cha miaka mitano katika Vita vya Pili vya Dunia, inazidisha mshtuko kwa kuzingatia kuwa asilimia 75 ya waliouawa ni wanawake, watoto, na wazee".

Umoja wa Mayahudi wa Ufaransa kwa ajili ya Amani umekosoa pia kisingizio cha "upotoshaji wa kutisha" kinachotumiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel cha kudai kwamba lengo la mashambulio unayofanya ni "kuiangamiza" Hamas, na kusisitiza kwamba lengo halisi la Tel Aviv ni kuendesha "vita vya kuangamiza idadi ya wakazi wa Gaza."

Kwa kuongezea, UJFP imeashiria pia uhamaji usio na mwisho wa Wapalestina wanaotaabishwa na Israel na kukoseshwa chakula, bomoabomoa na uharibifu unaofanywa katika kambi za Jenin na Huwara katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, pamoja na mateso makubwa yanayowapata wafungwa Wapalestina.

Kutokana na hali hiyo, Umoja wa Mayahudi wa Ufaransa kwa ajili ya Amani umewahutubu Wayahudi duniani kote ukisisitiza juu ya kuwepo sheria za kimataifa na haki za binadamu na kuwahimiza kuchukua msimamo wa pamoja wa kujipambanua na Israel ili kutoshirikishwa katika mauaji ya kimbari yanayoendelea Gaza".../

Tags