Jan 13, 2024 11:49 UTC
  • Ufaransa 'yaogopa' kujiunga na US, UK katika hujuma dhidi ya Yemen

Serikali ya Ufaransa imekataa kusaini taarifa ya kuunga mkono mashambulizi ya anga ya Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen, na kusisitiza kuwa haitashiriki katika hujuma hizo eti za kulinda safari za meli katika Bahari Nyekundu.

Paris imejiunga na Italia na Uhispania ambazo pia zimekataa kujiunga na muungano huo vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Marekani, sambamba na kukataa kusaini taarifa ya kuunga mkono hujuma hizo.

Shirika la habari la Iran Press limeripoti habari hiyo leo Jumamosi na kuongeza kuwa, serikali ya Rais Emmanuel Macron imekataa kushirikiana na waitifaki wake wa Magharibi dhidi ya Yemen, kama ilivyofanya wakati nchi wanachama wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) zilipoivamia Libya mwaka 2011. 

Wakati huo huo, Misri imeeleza kutiwa wasi wasi na kuongezeka operesheni za kijeshi katika eneo la Asia Magharibi na hujuma za anga za Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imeeleza kuwa, kuna haja kuwepo juhudi za pamoja za kupunguza taharuki, mivutano na ukosefu wa uthabiti katika eneo.

Serikali ya Cairo imeonya kuwa, hujuma hizo za anga za US na UK dhidi ya Yemen yumkini zikachochea na kushadidisha migogoro katika eneo hili la kistratajia.

Mashambulio hayo ya Marekani na Uingereza yamekabiliwa na radiamali na malalamiko ya nchi mbalimbali zikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia, China, Uturuki na Iraq na baadhi ya wabunge wa Marekani, ambao mbali na kukosoa kufanywa mashambulio hayo bila ya White House kuwa na kibali, wametahadharisha pia juu ya matokeo yake hasi.

Tags