Mtaalamu wa UN: Hakuna kinachoweza kuhalalisha ilichokifanya Israel Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i107400-mtaalamu_wa_un_hakuna_kinachoweza_kuhalalisha_ilichokifanya_israel_gaza
Mtalaamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameashiria ukiukaji wa sheria za kimataifa uliofanywa mara chungu nzima na utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa, hakuna kitu kinachoweza kuhalalisha vita vya mauaji ya kimbari vya Israel katika eneo hilo lilozingirwa.
(last modified 2024-01-19T08:17:18+00:00 )
Jan 19, 2024 08:17 UTC
  • Mtaalamu wa UN: Hakuna kinachoweza kuhalalisha ilichokifanya Israel Gaza

Mtalaamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameashiria ukiukaji wa sheria za kimataifa uliofanywa mara chungu nzima na utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa, hakuna kitu kinachoweza kuhalalisha vita vya mauaji ya kimbari vya Israel katika eneo hilo lilozingirwa.

Francesca Albanese, Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Palestina alisema hayo jana Alkhamisi akihutubia waandishi wa habari mjini Madrid na kuongeza kuwa, ukanyagaji wa sheria za kimataifa uliofanywa na Israel umeiweka Ukanda wa Gaza chini ya vita vya maangamizi ya kizazi kwa zaidi ya miezi mitatu sasa.

Mtalaamu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, utawala wa Israel unapasa uheshimu sheria ya kimataifa ya binadamu, lakini badala yake umeendelea kufanya mashambulizi ya mabomu dhidi ya Gaza, na katika wiki mbili tu za kwanza, ulitumia mabomu 12,000 yenye uzani wa pauni 2,000 (takriban kilo 907).

Albanese ameeleza bayana kuwa, "Mashtaka yatahitajika. Wahalifu ambao wamepanga, kuamuru na kutekeleza uhalifu kama huo lazima wafikishwe mahakamani." Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa: "Mahakama za kitaifa zenye mamlaka ya uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya kimbari lazima zianzishwe, kwani ICC inadhihirisha haichukui hatua za haraka kuhusu hali ya Palestina." 

Mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu wameyataja mashambulizi yanayoendelea ya utawala wa  Israel dhidi ya raia Wapalestina huko Gaza na vitendo vya adhabu ya pamoja kuwa ni "mauaji ya halaiki au mauaji ya kimbari".

Kushindwa Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, Karim Khan kuchukua hatua za kuzuia mauaji hayo ya kimbari kama vile kutoa hati za kukamatwa waliohusika na jinai hizo, akiwemo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, kumekosolewa vikali na viongozi mbalimbali kote duniani.

Utawala pandikizi wa Israel umeendelea kufanya mashambulizi ya anga na nchi kavu huko Gaza tangu Oktoba 7 mwaka jana na kuua Wapalestina zaidi ya 24,700 na kujeruhi wengine zaidi ya 60,000.