Feb 07, 2024 03:48 UTC
  • Biden aboronga tena, mara hii adai alikutana karibuni na Rais wa Ufaransa aliyefariki dunia 1996

Rais Joe Biden wa Marekani ameboronga tena kwa kumchukulia Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuwa ni rais wa zamani wa nchi hiyo marehemu Francois Mitterrand, alipokuwa akielezea yaliyojiri katika mkutano wa 2021 wa G7 wakati wa kampeni za uchaguzi mwishoni mwa juma.

Akihutubia mjini Las Vegas, Biden alikumbusha kuwa muda mfupi baada ya kuchaguliwa kuwa rais alielekea kusini mwa Uingereza kukutana na wakuu wa serikali nyingine sita mashuhuri za uchumi wa Magharibi, ambao aliwaita kimakosa kuwa ni "viongozi wote wa NATO."

“Nilikaa chini na nikasema, ‘Marekani imerudi tena.’ Na Mitterrand, kutoka Ujerumani – namaanisha, kutoka Ufaransa – akanitazama na kusema – akasema, ‘unajua, nini – kwa nini – umerudi kwa muda gani?”, alieleza rais huyo wa Marekani katika hali ya ubabaikaji.

Mitterrand aliwahi kuwa rais wa Ufaransa kuanzia 1981 hadi 1995 na alifariki dunia mwaka mmoja baada ya kuondoka madarakani, akiwa na umri wa miaka 79. Nakala rasmi ya hotuba ya Biden katika Ikulu ya White House inamtambulisha mtu ambaye alizungumza naye kwenye hafla ya G7, iliyofanyika Cornwall Juni 2021, kuwa ni Emmanuel Macron, rais wa sasa wa Ufaransa.

Biden

Kiongozi huyo wa sasa wa Marekani ni maarufu kwa kuboronga, akionyesha usahaulifu katika uzungumzaji kwa kutoa maelezo yasiyo sahihi na hata katika utembeaji, huku wakosoaji wake wakitoa angalizo kwamba matukio kama hayo yanazidi kuwa ya mara kwa mara kila uchao, na kuyataja kama ushahidi wa kuzorota kwa akili ya mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 81.

Wakati wa hotuba hiyo hiyo ya siku ya Jumapili, Biden alipongeza mradi wa dola bilioni tatu wa wa ujenzi wa reli ya kasi, iliyowekwa kuunganisha Las Vegas na Los Angeles. Rais huyo wa Marekani alisema watu wataweza kusafiri "kutoka hapa hadi Las Vegas" katika masaa mawili, kabla ya kujirekebisha na kueleza kuwa ni kutoka hapo Las Vegas hadi Los Angeles.../

 

 

Tags