Feb 09, 2024 11:04 UTC
  • Hukumu ya kutimuliwa nchini Sweden mhalifu aliyevunjia heshima Qur'ani Tukufu

Mahakama ya Uhajiri ya Sweden imetangaza kwamba, mtafuta hifadhi wa Iraq, ambaye amefanya vitendo kadhaa vya kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu, atafukuzwa nchini humo.

Ripoti zinasema serikali ya Sweden hatimaye imeamua kumfukuza Salwan Momika, mkimbizi kutoka Iraq, kwa sababu ya kukabiliwa na msimamo mkali na malalamiko ya kidiplomasia na ya Waislamu karibu bilioni mbili kote duniani kutokana na kuendelea kumkingia kifua mhalifu huyo aliyevunjia hehima Qur'ani Tukufu, na ilikuwa ikikaribia kutumbukia kwenye mgogoro mkubwa wa kidiplomasia na kiuchumi.

Hii ni pamoja na ukweli kwamba, Wasweden wengi hawakubaliani na kuchomwa moto nakala za kitabu kitakatifu cha Qur'ani, na zaidi ya nusu ya waliohojiwa katika kura ya maoni ya hivi majuzi ya Mtandao wa Umma wa Sweden walisema wanaunga mkono marufuku ya kuchomwa vitabu vitakatifu kama Qur'ani.

Oktoba mwaka jana (2023) Idara ya uhamiaji ya Sweden ilikataa kuongeza muda wa kibali cha kuishi nchini humo Salwan Momika, lakini amri yake ya kuondolewa ilicheleweshwa kwa sababu za kiusalama.

Uamuzi huu ulitolewa baada ya kubainika kuwa Momika alikuwa ametoa taarifa za uongo katika takwa lake la kuomba hifadhi.

Momika Salwan mwenye chuki na Uislamu

 

Mvunjiaji heshima huyo wa Qur’ani Tukufu alikata rufaa dhidi ya uamuzi huo, lakini rufaa yake ilikataliwa na majaji wa Uswidi. Kwa mujibu wa uamuzi huo, majaji waliamua kumpa Momika kibali cha muda cha kukaa ambacho muda wake unatarajiwa kumalizika Aprili 16 mwaka huu.

Salwan Momika, ambaye alichoma moto kitabu kitakatifu cha Qur’ani katika sikukuu ya Eidul Adh’ha mbele ya msikiti mkuu wa Stockholm kwa tamaa ya  kupata uraia wa Sweden, hivi karibuni alidai kwamba polisi wa Uswidi hawakumuunga mkono tena na kumfanya kuwa mawindo rahisi kwa Waislamu.  Hata hivyo mhalifu huyo alirudia kitendo cha kuchoma moto nakala ya Qur’ani tukufu mara kadhaa na kila mara alipatiwa himaya na uungaji mkono kamili wa polisi.

Inaonekana kuwa, licha ya uungaji mkono wa mara kwa mara wa serikali na polisi ya Sweden kwa Salwan Momika katika kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu, lakini mashinikizo ya nchi za Kiislamu na hata Umoja wa Mataifa kwa upande mmoja, na vikwazo dhidi ya Sweden na nchi za Kiislamu kwa upande mwingine dhidi ya nchi hiyo ya Skandinavia ni mambo ambayo yamewafanya maafisa wa nchi hiyo kuamua kuachana haraka na shari ya mhalifu huyo.

Katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya nchi za Ulaya hususan za eneo la Skandinavia zimekuwa uwanja wa ukiukaji na kuvunjiwa heshima matakatifu ya Waislamu. Tangu mwanzoni mwa majira ya kiangazi ya 2023, kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu kwa namna ya uchomaji Qur'ani kumetokea mara nyingi katika nchi mbili za kaskazini mwa Ulaya, yaani Sweden na Denmark, na baadhi ya watu wenye chuki dhidi ya Uislamu kama vile Salwan Momika na wafuasi wa vyama vya mrengo wa kulia vyenye misimamo ya kufurutu ada.

Maandamano dhidi ya vitendo vya Momika Salwan vya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu

 

Chini ya himaya na usaidizi wa polisi ya Sweden na Denmark, watu hawa walichoma moto Quran Tukufu na maandamano ya Waislamu ya kulaani vitendo hivyo pia yalizimwa na kukandamizwa. Baada ya Salwan Momika kuitusi Quran Tukufu, ubalozi wa Uswidi mjini Baghdad ulishambuliwa na waandamanaji wenye hasira na kuchomwa moto.

Kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu kumekabiliwa na wimbi la malalamiko makubwa hususan katika ulimwengu wa Kiislamu na kupelekea maandamano makubwa katika ulimwengu wa Kiislamu na nchi nyinginezo. Kuhusiana na hilo  hivi karibuni Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ilizitaka nchi wanachama kuchukua hatua zinazofaa za kisiasa na kiuchumi dhidi ya Uswidi na nchi nyinginezo ambazo zinaruhusu kuchomwa vitabu vitakatifu vya Kiislamu.

Mapema Julai 2023, Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lililaani kutusiwa na kuvunjiwa heshima Qur'ani kwa kuidhinisha azimio lililopendekezwa na nchi za Kiislamu na kumtaka Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu kuchunguza suala hilo na kutoa ripoti.

Licha ya kuwepo kwa radiamali kubwa ya Waislamu na nchi za Kiislamu kuhusu suala la Qur'ani kuchomwa moto katika nchi mbili za kaskazini mwa Ulaya, yaani Sweden na Denmark, na upinzani wa wazi wa Umoja wa Mataifa dhidi ya kitendo hiki cha dharau na kisichokubalika na hata ahadi za mamlaka za nchi hizi mbili za kuzuia vitendo hivyo, lakini watu wenye chuki dhidi ya Uislamu wameendelea kuvunjia heshima kitabu kitakatifu cha Qur'ani kwa uhuru na himaya kamili ya vyombo vya usalama.

Himaya na uungaji mkono wa Wamagharibi kwa kitendo cha kuvunjiwa heshima na cha kuchomwa moto Qur'ani unafanyika katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa unapinga kitendo hicho cha aibu. Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa anasema: Miguel Moratinos, Mkuu wa Asasi ya Staarabu ya Umoja wa Mataifa amelaani vikali kuchomwa moto Qur'ani Tukufu mbele ya msikiti mmoja katikati ya mji wa Stockholm, Sweden.

Waandamanaji wakiwa na ujumbe usemao: Kuchoma moto Qur'ani ni ugaidi

 

Inaonekana kuwa, Wamagharibi wanapuuza kwa makusudi tofauti baina ya uhuru wa kusema na kutusi matukufu ya dini. Tukitupia jicho vigezo vya kindumakuwili vya madola Magharibi zikiwemo Sweden na Denmark kuhusiana na uhuru wa kutoa maoni tunaona kuwa, jambo hili hubeba maana pale tu linapohoji na kuvunjia heshima jambo ambalo ndio mtazamo wa Magharibi kama vile chuki dhidi ya Uislamu na kuvunjia heshima matukufu ya Waislamu. Lakini mambo ni kinyume kabisa kuhusiana na masuala mengine kama vile ngano ya Holocaust.

Mfano mwingine wa wazi ni kadhia ya haki za binadamu na ugaidi ambapo unafiki wa madola ya Magharibi unaonekana bayana katika masuala haya.

Tags