Mar 14, 2024 07:10 UTC
  • Ripota wa UN: Israel imeua watoto wengi zaidi Ukanda wa Gaza miezi mitano iliyopita

Francesca Alnanese Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina alisema jana katika ripoti kali iliyowasilishwa kwa umoja huo kuwa Israel imeua watoto wengi zaidi katika Ukanda wa Gaza katika kipindi cha miezi mitano iliyopita.

Amesema idadi hiyo ya vifo ni kubwa kuwahi kushuhudiwa katika mizozo yote duniani iliyojiri katika kipindi cha miaka minne ya karibuni. Francesca Albanese amekosoa hali ya mgogoro inayousibu Ukanda wa Gaza na kusema kuwa kile kinachojiri katika eneo hilo ni mchakato wa kimfumo ambao ni sawa na mauaji ya kimbari. 

Ripoti ya Albanese inasisitiza kuhusu hali halisi ya kutisha inayowakabili watoto wa Kipalestina chini ya uvamizi wa Israel, ikionyesha hali mbaya ya mzozo huo. Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ameandika katika ukurasa wake wa X kwamba: "Kuangamiza idadi ya watu kutoka kwenye asili yake. Mauaji ya kimbari ni mchakato, na kinachotokea Gaza ni janga lililotabiriwa."

Watoto wa Gaza na mashambulizi ya kikatili ya Israel 

Ripoti hiyo kali ya Francesca Albanese kwa Umoja wa Mataifa imeweka wazi mashambulizi yasiyosita ya Israel dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza khususan watoto ambao ni wahanga wakuu wa jinai hizo. 

Zaidi ya Wapalestina 31,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto wameuawa shahidi huko Gaza, na wengine zaidi ya 73,000 kujeruhiwa tangu utawala haramu wa Kizayuni uanzishe mashambulizi ya kikatili dhidi ya eneo hilo Oktoba 7 mwaka jana huku kukiwa na uharibifu mkubwa wa miundombinu, ukosefu wa chakula na mahitaji mengine muhimu. 

Tags