Mar 25, 2024 02:12 UTC

Kijana Muislamu mwenye umri wa miaka 15 aliyeokoa zaidi ya watu mia moja wakati wa hujuma ya kigaidi kwenye ukumbi wa tamasha wa Crocus City Hall nje kidogo ya jiji la Moscow, siku ya Ijumaa iliyopita, ametunukiwa nishani ya ushujaa.

Hatua hiyo imechukuliwa na Idara ya Dini ya Kiislamu na Baraza la Mufti wa Russia ambayo imetangaza kwamba, Islam amepewa tuzo ya ushujaa ili kuenzi kazi nzuri ya kijana huyo Mrusi.

Magazeti ya Nezavisimaya Gazeta na Kommersant ya Russia yameripoti kuwa, mwanafunzi "Islam" mwenye umri wa miaka 15 alikuwa akifanya kazi katika chumba cha kubadilishia nguo cha jumba la biashara la Crocus City Hall katika viunga vya Moscow, na baada ya kusikia sauti za risasi alikimbilia kusaidia watu na kuwaelekeza katika njia ya dharura ili kutoka nje ya jumba hilo.  Zaidi ya watu mia moja walinusuriwa na kiijana huyo Muislamu wa Russia.

Katika akaunti yake kwenye jukwaa la X, Shirika la Habari la Sputnik limemtaja kijana Islam kuwa ni shujaa halisi aliyeokoa maisha ya watu mia moja katika hujuma ya kigaidi ya Crocus City Hall.

Shambulizi la kigaidi Crocus City Hall, Moscow

Televisheni ya Russia Today pia imerusha hewani mahojiano yake na kijana Islam, ambaye amesema: "Ni bora kufa vitani kuliko kuwaacha watu wengine wauawe." 

Baba wa kijana huyo amesema: "Islam alikuwa akifanya kazi kwa muda katika jumba hilo la kibiashara na kwamba eneo lake la kazi lilikuwa kwenye ghorofa ya chini ya jengo, ambako alikimbilia kufungua milango kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu."

Tags