Mar 28, 2024 10:08 UTC
  • UN: Khumsi moja ya chakula duniani inaishia jaani wakati watu milioni 783 wanalala na njaa

Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira UNEP imesema, wakati theluthi moja ya watu duniani wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, milo bilioni moja, ambayo ni sawa na moja ya tano ya chakula chote hutupwa kila siku na kuishia jalalani.

Ripoti hiyo ya UNEP, ambayo imetolewa kwa anuani ya “Kielelezo cha Taka za Chakula 2024” inaangazia takwimu za hivi karibuni kuanzia mwaka 2022 ambazo zinaonyesha kuwa tani bilioni 1.05 za chakula zilipotea.

Asilimia 19 ya chakula ambacho kipo kwa ajili ya watumiaji kilipotea kwa jumla katika maduka ya rejareja, sekta ya huduma ya chakula na viwango vya kaya.

Hiyo ni pamoja na karibu asilimia 13 ya chakula kilichopotea katika mnyororo wa usambazaji, kama inavyokadiriwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO kuanzia tu baada ya mavuno hadi katika hatua ya kuuzwa.

Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP amesema: “upotevu wa chakula ni janga la kimataifa. Mamilioni ya watu watakuwa na njaa leo huku chakula kikiharibika kote duniani”.

Inger Andersen

Ripoti hiyo ya UNEP inasema, takataka nyingi za chakula duniani zinatokana na kaya, jumla ya tani milioni 631 au hadi asilimia 60 ya jumla ya chakula kilichotupwa. Sekta ya huduma ya chakula na biashara ya rejareja imewajibika kwa tani milioni 290.

Kwa mujibu wa waandishi wa ripoti hiyo ya UNEP kwa wastani, kila mtu hupoteza kilo 79 za chakula kila mwaka. Hii ni sawa na mlo 1.3 kila siku kwa kila mtu ulimwenguni aliyeathiriwa na njaa.

Ripoti hiyo iliyochapishwa kabla ya Siku ya Kimataifa ya kutotupa taka inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 30 Machi mwaka huu ikibeba anuani: “Tathimini ya uchafuzi wa taka za Chakula”, imeandaliwa kwa ushirikiano na WRAP, NGO ya Uingereza inayoshughulikia masuala ya tabianchi.../

Tags