Apr 11, 2024 09:54 UTC
  • Russia yataka kutekelezwa haraka amri ya Umoja wa Mataifa ya kukomeshwa vita Ghaza

Russia imetaka kutekelezwa haraka na bila ya masharti azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kusimamishwa mara moja mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Ghaza.

Shirika la habari la Anadolu limemnukuu Maria Zakharova, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia akisema hayo na kusisitiza kuwa, maazimio ya Baraza la Usalama likiwemo lile la 2728 lililopasishwa mwezi Machi mwaka huu la kuitaka Israel ikomeshe mara moja mashambulizi yake huko Ghaza, ni lazima yaheshimiwe na wanachama wote wa Umoja wa Mataifa.

Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amelalamikia pia madai ya mwakilishi wa Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa aliyedai kuwa baadhi ya vipengee vya azimio hilo si lazima kutekelezwa na kusisitiza kuwa, msimamo huo wa Marekani unaonesha wazi namna Washington na madola ya Magharibi yanayounga mkono na kusaidia jinai na mauaji ya kimbari huko Ghaza na kwamba madola hayo ya Magharibi hayajali sheria bali yanafanya kile yanachokipenda.

Simamisheni haraka mauaji ya kimbari

 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amezungumzia pia shambulizi la hivi karibuni la utawala wa Kizayuni dhidi ya sehemu ya ubalozi mdogo wa Iran katika mji mkuu wa Syria, Damascus na  kusisitiza kuwa, shambulio hilo linakanyaga waziwazi maazimio na hati ya Umoja wa Mataifa, na kwamba viongozi wa Israel wanaweza kuchukuliwa hatua kali kwa namna tofauti ikiwa ni pamoja na jamii ya kimataifa, lakini madola ya Magharibi yanazuia jambo hilo. 

Duru za hospitali za Palestina zinasema kuwa, hadi hivi sasa zaidi ya Wapalestina 33,000 wameshauliwa shahidi na zaidi ya 76,000 wengine wameshajeruhiwa katika jinai za hivi sasa za Israel huko Ghaza.

Tags