May 23, 2024 07:44 UTC
  • Seneta wa Marekani aunga mkono ICC kutoa waranti wa kuwakamata viongozi wa Israel

Seneta wa Marekani Bernie Sanders amesema anaunga mkono maombi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) Karim Khan ya kutaka viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wakamatwe na ameitaka Marekani iheshimu sheria za kimataifa.

Sanders ameieleza Seneti: "nionavyo ni kwamba ICC inajaribu kuzingatia sheria za kimataifa na kuinua viwango (alau) vya chini vya heshima. Serikali yetu isifanye chini ya hivyo". 
 
Kauli ya seneta huyo imekuja baada ya Khan kuomba hati ya kukamatwa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wa vita wa utawala huo wa Kizayuni Yoav Gallant kwa kuhusika na "uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu" uliofanywa na jeshi la Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza.
 
Sanders amesema wakati ICC ilipomtangaza Rais wa Russia Vladimir Putin kuwa mhalifu wa vita mwaka jana, serikali ya Marekani ilikaribisha uamuzi wake.
Bernie Sanders

Amefafanua kwa kusema: "baadhi wamehoji kuwa si haki kumlinganisha mkuu aliyechaguliwa kidemokrasia wa serikali ya Israel na Putin, ambaye anaendesha mfumo wa kimabavu...ndiyo, viongozi waliochaguliwa kidemokrasia (pia) wanaweza kufanya uhalifu wa kivita".

 
Seneta Sanders amesisitiza kwa kusema: "ICC inafanya kazi yake. Inafanya kile inachopaswa kufanya. Hatuwezi kutumia sheria za kimataifa pale tu zinapoturidhisha".
 
Amewakumbusha maseneta wa Marekani kwamba zaidi ya Wapalestina 35,000 wameuawa na karibu 80,000 wamejeruhiwa tangu vilipoanza vita vya kinyama vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ghaza tarehe 7 Oktoba mwaka jana.../

 

Tags