Waislamu wanasherekea siku ya kupewa Utume Nabii Muhammad (saw)
Waislamu katika pembe mbalimbali za dunia leo wanaadhimisha kumbukumbu ya kubaathiwa na kupewa Utume, Nabii Muhammad (saw).
Sikukuu ya Mab'ath ni siku ambayo Muhammad bin Abdullah (saw) aliteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mtume wake wa Mwisho akiwa katika pango la Hira huko Makka, baada ya kukamilisha umri wa miaka 40.
Muhammad (saw) aliteuliwa kuwa Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, tarehe 27 Rajab katika Mwaka wa 40 wa Tembo ili kuiokoa jamii ya mwanadamu, ambayo ilikuwa imezama katika ujinga na ufuska, na kuielekeza kwenye maadili mema, utu na ubinadamu.
Siku hii ya kupewa Utume Nabii Muhammad (saw) inapaswa kutambuliwa kuwa mwanzo wa kuundwa ustaarabu mkubwa zaidi duniani, ambao uliokoa wanadamu kutokana na fikra na imani potofu.
Muujiza mkubwa zaidi wa Mtume Muhammad (saw) ni kitabu kitakatifu cha Qur'ani kilichosababisha mageuzi makubwa ya kifikra na kiutamaduni na kumfungulia mwanadamu mlango wa kumjua vyema Mungu na kujitambua vizuri yeye mwenyewe.

Kwa kutumia kitabu hicho, Muhammad (saw) aliwafundisha wanadamu fikra mpya na aali kama vile kuheshimu na kuwakirimu wanawake waliokuwa wakizikwa wakiwa hai katika zama hizo, kupigana dhidi ya dhulma na ibada ya masanamu, kuwasaidia wanadamu wenzetu, imani ya Tauhidi na kumwabudu Mungu Mmoja na maadili mema, na kuwaonyesha wanadamu njia ya kupata saada na ufanisi hapa duniani na huko Akhera.
Nchini Iran usiku wa kuamkia leo miji mbalimbali imeshuhudia sherehe na maadhimisho ya kumbukumbu ya kubaathiwa na kupewa Utume mbora wa viumbe, Mtume Muhammad (saw).
Hapa nchini Iran pia siku hii ya kumbukumbu ya kupewa Utume Muhammad (saw) inaadhimishwa kama sikukuu kubwa na huwa siku ya likizo ya kitaifa kwa ajili ya kusherehekea tukio hilo adhimu lililobadili dunia na historia ya mwanadamu.