Hatua ya Trump yaitafakarisha Kenya juu ya operesheni ya Haiti
(last modified Wed, 05 Feb 2025 12:18:16 GMT )
Feb 05, 2025 12:18 UTC
  • Hatua ya Trump yaitafakarisha Kenya juu ya operesheni ya Haiti

Kenya imesema imeanzisha mchakato wa kubadilisha ujumbe wake wa usalama ulioko Haiti kuwa operesheni ya Umoja wa Mataifa, baada ya Marekani kusimamisha ufadhili kwa ujumbe huo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Kenya, Korir Sing’oei amesema kuwa, licha ya Marekani kuzuia ufadhili huo kwa muda wa siku 90, lakini ujumbe huo wa kudumisha amani nchini Haiti unaendelea kufanya kazi kwa kutumia rasilimali zilizopo.

Katika mahojiano na shirika la habari la Anadolu, Sing'oei amekosoa hatua hiyo ya Marekani ya kusimamisha ufadhili kwa shughuli mbali mbali za kimataifa. "Hakuna msingi wowote kwa Marekani kuiagiza UN kuzuia ufadhili, hakuna msingi kabisa." 

Amesisitiza kuwa, ujumbe huo tayari una akiba ya dola milioni 110 za kuendelea na shughuli zake, na kwamba wana imani kubwa kwamba nchi nyingine zitajitokeza kufadhili mpango huo.

Rais Ruto akiaga na wanajeshi wa Kenya waliotumwa Haiti

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Kenya ilituma maafisa 217 zaidi wa polisi nchini Haiti, kama sehemu ya jeshi la kimataifa la kukabiliana na ghasia za magenge katika taifa hilo la Carribbea. Kenya ilituma wanajeshi wake Haiti kwa mara ya kwanza mwezi Juni mwaka jana, na kufikia sasa imetuma zaidi ya wanajeshi 600.

Rais William Ruto aliahidi kupeleka wanajeshi 1,000 kama sehemu ya kikosi kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa nchini Haiti. Kwa mujibu wa UN, zaidi ya watu 5,600 waliripotiwa kuuawa kote nchini Haiti mwaka juzi, kabla ya kutumwa vikosi vya kimataifa vikiogozwa na Kenya.