Waziri Mkuu wa Ufaransa aunga mkono marufuku ya 'burqini'
(last modified Thu, 18 Aug 2016 03:39:30 GMT )
Aug 18, 2016 03:39 UTC
  • Waziri Mkuu wa Ufaransa aunga mkono marufuku ya 'burqini'

Waziri Mkuu wa Ufaransa ameunga mkono hatua ya mameya wa miji minne nchini humo kupiga marufuku vazi la stara la kuogelea linalovaliwa na wanawake wa Kiislamu linalofahamika kama 'burqini'.

Manuel Valls amesema vazi hilo haliendani na thamani, utamaduni na desturi ya Wafaransa na hivyo ni sawa kwa wanawake wa Kiislamu kutoruhusiwa kulivaa wanapoenda kuogelea kwenye fukwe za umma.

Waziri Mkuu wa Ufaransa amedai kuwa, vazi hilo linaashiria misimamo fulani ya kisiasa, linahujumu mila za jamii za Wafaransa na ambalo linaunga mkono utumwa dhidi ya wanawake.

'Burqini'

Jumanne iliyopita, Meya Michel Py wa mji wa Leucate, katika pwani ya Ufaransa alitangaza kupiga marufuku vazi hilo la burqini, eti kwa kuwa linaunga mkono utamaduni wa kidini na yumkini jambo hilo likawachukiza au kuwashtua watu wa dini nyingine.

Aidha Daniel Fasquelle, Mkuu wa mkoa wa Touquet ametangaza kupiga marufuku vazi hilo linalomsitiri mwanamke wa Kiislamu anapoogelea katika fukwe za umma.

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Julai, David Lisnard, Meya wa mji wa Cannes, kusini mwa Ufaransa, alikuwa kiongozi wa kwanza kupiga marufuku uvaaji wa burkini, akisisitiza kuwa kuna haja ya kuvaa nguo za kawaida zisizoashiria misimamo ya kidini ufukweni.

Tags