UN: Watoto 75 elfu wapo katika hatari ya kufa njaa Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/world-i16330-un_watoto_75_elfu_wapo_katika_hatari_ya_kufa_njaa_nigeria
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa, maelfu ya watoto wadogo wapo katika hatari ya kupoteza maisha katika kipindi cha mwaka mmoja ujao, kutokana na njaa na utapiamlo 'uliosababishwa' na kundi la wanamgambo wa Boko Haram.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 29, 2016 13:54 UTC
  • UN: Watoto 75 elfu wapo katika hatari ya kufa njaa Nigeria

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa, maelfu ya watoto wadogo wapo katika hatari ya kupoteza maisha katika kipindi cha mwaka mmoja ujao, kutokana na njaa na utapiamlo 'uliosababishwa' na kundi la wanamgambo wa Boko Haram.

Arjan de Wagt, Mkuu wa masuala ya lishe wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) amesema kuwa, watoto zaidi ya 75,000 wanakabiliwa na hatari ya kuaga dunia kutokana na njaa na utapiamlo haswa katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria.

UNICEF imesema inahitaji dola milioni 115 za Marekani ili kunusuru maisha ya watoto hao. Mkuu wa masuala ya lishe wa UNICEF ameongeza kuwa, licha ya idadi kubwa ya watoto kuendelea kupoteza maisha kutokana na njaa na utapiamlo nchini Nigeria, wafadhili wametoa dola milioni 24 tu kati ya dola 115 zinazohitajika.

UNICEF: Watoto 75,000 wanahitaji msaada wa dharura Nigeria

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Agosti, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa ulitangaza kwa masikitiko kuwa, robo ya mashambulizi ya kigaidi ya kundi la Boko Haram yanafanywa na watoto haswa katika eneo la Ziwa Chad linalojumuisha nchi za Chad, Cameroon, Niger na Niger.

Wanamgambo wa Boko Haram wamekuwa wakitumia watoto wadogo katika hujuma zao za kigaidi

Mkurugenzi wa Unicef katika kanda ya magharibi na katikati mwa Afrika, Manuel Fontaine amesema kuwa, watoto 38 wametumiwa na kundi la Boko Haram kufanya mashambulizi ya kijilipua kwa mabomu tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2016 na 86 wametumiwa kujilipua kwa mabomu tangu mwaka 2014 hadi sasa katika eneo la Ziwa Chad.