Wito wa kimataifa wa kudhamini usalama wa wakimbizi
Taasisi kadhaa za kimataifa zimetoa wito wa kudhaminiwa usalama na kulindwa maisha ya wakimbizi wanaojaribu kuingia Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranea.
Taasisi hizo ambazo ni Shirika la Kimataifa la Wahajiri IOM, Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa UNHCR na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF zimetoa taarifa ya pamoja na kusema kuanzia mwezi Septemba mwaka 2015, kwa wastani watoto wawili wamekuwa wakizama na kupoteza maisha kila siku mashariki mwa Bahari ya Mediterranea. Anthony Lake Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF amesema pengine hakuna matumaini ya kuwazuia watu kupitia bahari wakikimbia nchi zenye migogoro lakini kwa ushirikiano kuna uwezekano wa kuondoa hatari katika safari za wakimbizi.
Kwa upande wake, mkuu wa UNHCR Filippo Grandi amebainisha masikitiko yake kufuatia kupoteza maisha wakimbizi wakati boti zao zinapoghiriki idadi kubwa ya wakimbizi wakiwa njiani kuelekea Ulaya. Kwa msingi huo ametoa wito kwa nchi za Ulaya kuweka njia rasmi na zenye usalama ili wakimbizi wasipoteze maisha wakiwa njiani. Katika wiki saba za kwanza za mwaka 2016, kati ya wakimbizi zaidi ya laki nane ambao walikuwa wakipitia Bahari ya Mediterranea wakielekea Ulaya takribani wakimbizi 410 walipoteza maisha idadi ambayo ni mara 35 zaidi ya waliopoteza maisha mwaka 2015. Watoto walikuwa ni asilimia 36 ya waathirika wa janga hilo.
Pamoja na kuwepo ombi la taasisi za kimataifa kuhusu kulindwa maisha ya wakimbizi, hakujakuwepo na maelewano baina ya nchi za Ulaya kuhusu namna na kuwashughulikia wakimbizi. Ujerumani na nchi zingine za Ulaya zimeonya dhidi ya kulazimishwa kuwakubali wakimbizi.
Thomas de Maizière Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani siku ya Ijumaa alizungumza mbele ya bunge la nchi hiyo akizihutubu nchi za Ulaya na kusema nchi yake haitakubali kushurutishwa kuwakubali wakimbizi. Waziri huyo wa Ujerumani amesema baadhi ya nchi za Ulaya zinajaribu kuipa Ujerumani mzigo wote wa wakimbizi katika hali ambayo hilo ni tatizo la pamoja la nchi zote za Umoja wa Ulaya. Aidha Thomas de Maizière amesema Ujerumani itachukua hatua kali zaidi kuhusu wakimbizi nchini humo. Uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa asilimia 58 ya Wajerumani wanaamini kuwa mipaka ya nchi hiyo inapaswa kudhibitiwa zaidi ili wakiimbizi wasipate mwanya wa kuingia. Ujerumani ina uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya na mwaka 2015 ilipokea wakimbizi milioni moja na laki moja, idadi ambayo ni kubwa zaidi barani humo.
Dimitry Medvydev Waziri Mkuu wa Russia amekosoa vikali sera za Ujerumani na Umoja wa Ulaya kwa ujumla kuhusu wakimbizi ambapo amesema sera hizo zimefeli. Amesema kuwawekea vizuizi malaki ya wakimbizi wanaotaka kuingia barani Ulaya ni jambo linalohatarisha usalama wa dunia.