Trump ashinda uchaguzi wa rais Marekani, masoko ya hisa yaporomoka
https://parstoday.ir/sw/news/world-i19120-trump_ashinda_uchaguzi_wa_rais_marekani_masoko_ya_hisa_yaporomoka
Masoko ya hisa ya dunia na hususan ya Marekani yameporomoka kwa kiasi kikubwa muda mfupi baada ya Donald Trump wa chama cha Republican kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 09, 2016 04:46 UTC
  • Trump ashinda uchaguzi wa rais Marekani, masoko ya hisa yaporomoka

Masoko ya hisa ya dunia na hususan ya Marekani yameporomoka kwa kiasi kikubwa muda mfupi baada ya Donald Trump wa chama cha Republican kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais nchini humo.

Trump mwenye umri wa miaka 70 ameibuka mshindi kwa kupata kura 270 kati ya kura 538 za wajumbe wa majimbo yote 50 ya Marekani, zilizohitajika kumpata mshindi.

Habari zaidi zinasema kuwa, Clinton licha ya kufanyiwa kampeni na Rais anayeondoka Barack Obama tayari amekubali kushindwa na kumpigia simu Trump kumpongeza kwa ushindi wake.

Clinton na Trump

Imearifiwa kuwa, thamani ya dola ya Marekani vile vile imeshuka kutokana na ushindi wa Trump huku wawekezaji wa kigeni nchini humo wakieleza hofu yao ya kutangazwa mshindi Trump, wakisisitiza kuwa hawajui hatima ya biashara zao na sera mpya za kigeni za mwanasiasa huyo tajiri. Hii ni kutokana na maneno yake makali kwa wageni na wahamiaji wakati wa kampeni zake.

Awali habari ziliarifu kuwa, mtu mmoja ameuawa na wengine wanne kujeruhiwa katika tukio la ufyatuaji risasi lililojiri katika jimbo la California. Ghasia hizo zilizotokea katika mji wa Azusa, yapata kilomita 40 mashariki mwa mji wa Los Angeles usiku wa kuamkia leo, zilisababishwa kufungwa vituo viwili vya kupigia kura.