Msomaji habari wa kwanza mwenye kuvaa Hijabu awavutia wengi Canada
Mwandishi habari wa kwanza wa kike kusoma habari akiwa amevaa vazi la Kiislamu la Hijabu nchini Canada amewavutia watu wengi nchini humo.
Kwa mujibu wa gazeti ya Guardian, Televisheni ya City News imekuwa kituo cha kwanza cha Televisheni nchini Canada kumtumia mwanamke Mwislamu aliyevaa Hijabu kusoma habari katika wakati muhimu.
Bi. Ginella Massa alitakiwa asome habari za saa tano usiku siku ya Ijumaa na hatua hiyo ikawavutia na kuwafurahisha wengi nchini humo.
Baada ya kutangaza taarifa hiyo ya habari, Massa aliandika katika mtandao wa Twitter kuwa, mwanamke Mwislamu anapovaa Hijabu huwa ni nembo ya Uislamu na huwa anafikisha ujumbe wenye nguvu.
Mwanamke huyo Mwislamu ambaye ni mwandishi habari amesema kuna umuhimu mkubwa kwa vyombo vya habari kueneza taswira sahihi kuhusu wanawake Waislamu.
Mafanikio hayo yanakuja huku kukiwa na ongezeko la vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu katika nchi jirani ya Marekani na barani Ulaya.