HRW: Serikali inaficha jinai na mauaji dhidi ya Waislamu wa Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/world-i22885-hrw_serikali_inaficha_jinai_na_mauaji_dhidi_ya_waislamu_wa_myanmar
Mashirika ya kutetea haki za binadamu ikiwemo Human Rights Watch yamesema serikali ya Myanmar inajaribu kuficha jinai na mauaji yanayofanywa na vikosi vya usalama vya nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa Rohingya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 05, 2017 16:09 UTC
  • HRW: Serikali inaficha jinai na mauaji dhidi ya Waislamu wa Myanmar

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ikiwemo Human Rights Watch yamesema serikali ya Myanmar inajaribu kuficha jinai na mauaji yanayofanywa na vikosi vya usalama vya nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa Rohingya.

Hii ni baada ya Kamisheni ya Uchunguzi iliyoongozwa na serikali kutoa ripoti hapo jana iliyodai kuwa, hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kuwa mauaji ya kimbari, ubakaji na jinai nyinginezo zimefanywa na askari wa nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa Rohingya. 

Akitoa radiamali yake kufuatia ripoti hiyo, Phil Robertson, Naibu Mkurugenzi wa Human Rights Watch katika eneo la Asia amesema: "Serikali ya Myanmar imetekeleza kile tulichokuwa na wasi wasi nacho, kujaribu kufumbia macho mauaji na jinai zinazofanywa na wanajeshi wake dhidi ya Waislamu wa Rohingya, magharibi mwa jimbo la Rakhine."

Msikiti ulioshambuliwa na kubomolewa na askari wa Myanmar

Naye Matthew Smith, muasisi wa vuguvugu la kutetea haki za binadamu liitwalo Fortify Rights amesema kuwa: "Ni wazi jinai za kutisha zimefanywa na wanajeshi wa Myanmar licha ya kamisheni hiyo ya uchunguzi kujaribu kuficha na kupotosha ukweli wa mambo; wizara zikiongozwa na Suu Kyi zimeanzisha kampeni za kipropaganda za kujaribu kuficha mauaji hayo ya kutisha."

Tangu mwaka 2012 Mabudha wenye misimamo mikali wakisaidiwa na maafisa usalama wa Myanmar wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali za ukatili, mauaji na kubaka wanawake Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini humo, kwa shabaha ya kuwalazimisha kuondoka katika nyumba na makazi yao hususan katika jimbo la Rakhine.

Mabudha wenye misimamo mikali

Serikali imekataa kuwapa uraia Waislamu wa jamii ya Rohingya wapatao milioni 1.1 na kuwataja kama wahamiaji haramu kutoka Bangladesh.