Morocco yapiga marufuku uzalishwaji na uuzaji wa burqa
(last modified Wed, 11 Jan 2017 15:20:22 GMT )
Jan 11, 2017 15:20 UTC
  • Morocco yapiga marufuku uzalishwaji na uuzaji wa burqa

Serikali ya Morocco imepiga marufuku uzalishaji na uuzaji wa vazi la burqa linalovaliwa na baadhi ya wanawake Waislamu nchini humo.

Ingawaje hakuna taarifa rasmi ya serikali iliyotolewa kuhusiana na sababu za kuchukuliwa uamuzi huo, lakini duru za habari zinasema kuwa agizo hilo la Wizara ya Mambo ya Ndani linatazamiwa kuanza kutekelezwa wiki hii.

Tovuti ya habari ya Le360 imemnukuu afisa wa ngazi za juu wa wizara hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina akisema kuwa, serikali imechukua hatua zote kuhakikisha kuwa vazi hilo haliingizwi katika masoko ya nchi hiyo kutoka nje, kuzalishwa wala kuuzwa.

Afisa huyo ameambia Le360 kuwa, serikali imechukua uamuzi kutokana na sababu za kiusalama na kusisitiza kuwa wahalifu wamekuwa wakifanya uhalifu wao wakiwa wamevalia vazi hilo la burqa.

Wanawake Waislamu waliovalia vazi l niqabu

Haya yanajiri siku chache baada ya Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel kutoa wito wa kupigwa marufuku vazi la burqa, linalovaliwa na wanawake wa Kiislamu. Akizungumza hivi karibuni mjini Essen wakati akizindua azma yake ya kuwania muhula mwingine wa uenyekiti wa Muungano wa Kikristo unaojulikana kama Christian Democratic Union (CDU), Merkel alisema vazi hilo la niqabu linapaswa kupigwa marufuku nchini humo akisisitiza kuwa sheria ya Ujerumani iko juu ya kanuni na sheria za kidini.

Mwezi Oktoba mwaka uliomalizika wa 2016, Bulgaria ilijiunga na baadhi ya nchi za Magharibi zilizopiga marufuku vazi la burqa kama vile Canada, Ubelgiji na Ufaransa, baada ya Bunge la nchi hiyo kupasisha sheria inayopiga marufuku vazi hilo linalovaliwa na wanawake Waislamu nchini kote.

Tags