Rais wa Ufaransa amtaka Trump aheshimu JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/world-i24411-rais_wa_ufaransa_amtaka_trump_aheshimu_jcpoa
Rais wa Ufaransa amemtaka Rais mpya wa Marekani aheshimu makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 yaliyosainiwa huko Vienna nchini Austria Julai mwaka 2015.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 29, 2017 10:21 UTC
  • Rais wa Ufaransa amtaka Trump aheshimu JCPOA

Rais wa Ufaransa amemtaka Rais mpya wa Marekani aheshimu makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 yaliyosainiwa huko Vienna nchini Austria Julai mwaka 2015.

Katika mazungumzo ya simu hapo jana, Rais Francois Hollande wa Ufansa amemtaka mwenzake wa Marekani Donald Trump kuheshimu makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA) baina ya Iran na madola sita makubwa duniani ambayo ni Marekani, China, Russia, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani.

Hollande amemtaka Trump azingatie taathira za baadaye za kisiasa na kiuchumu iwapo ataamua kuchukua hatua zozote za kukiuka makubaliano hayo ambayo yalianza kutekelezwa Januari mwaka jana.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa

Mwezi uliopita, Rais Hassan Rouhani alisisitiza kuwa Iran haitairuhusu Marekani ikiuke au iichane hati ya makubaliano ya nyuklia ya (JCPOA).

Ikumbukwe kuwa, wakati wa kampeni za uchaguzi, Trump alitishia kuyachana makubaliano ya nyuklia na Iran wakati atakapoingia katika ikulu ya Marekani, White House. Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alijibu msimamo huo wa Trump kwa kusema, makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hayawezi kuvunjwa kwa uamuzi wa serikali ya nchi moja.

Trump akisaini amri dhidi ya wakimbizi na wahamiaji

Wakati huo huo, Rais Francois Hollande wa Ufaransa amemtaka Trump aheshimu kadhia ya kuwakubali wakimbizi nchini humo, na kuongeza kuwa, azimio kuhusu mgogoro wa Syria linaweza kutekelezwa tu katika fremu ya Umoja wa Mataifa.