UN yaunda timu ya kuchunguza jinai dhidi ya Waislamu wa Rohingya
Umoja wa Mataifa umeunda timu ya wataalamu huru kuchunguza mauaji na jinai zinazofanywa na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya katika jimbo la Rakhine.
Taarifa iliyotolewa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa imesema timu hiyo yenye wataalamu watatu itaongozwa na Indira Jaising, wakili wa Mahakama ya Juu ya India.
Wataalamu wengine ni Radhika Coomaraswamy, wakili na mtetezi mkongwe wa haki za binadamu raia wa Sri Lanka na mwanaharakati wa Australia, Christopher Sidoti.
Mapema mwezi Machi mwaka huu, baraza hilo la UN lilikubali kuunda timu huru ya wataalamu kuchunguza madai hayo dhidi ya wanajeshi wa Myanmar, huku ikiwataka maafisa wakuu serikalini kushirikiana na timu hiyo katika uchunguzi wao.
Hii ni katika hali ambayo, wiki iliyopita, jeshi la Myanmar lilipinga vikali ripoti ya uchunguzi wa Umoja wa Mataifa iliyosema kuwa viongozi wa serikali wanabeba dhima ya jinai zilizotendwa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya.
Ripoti hiyo ya mwezi Februari mwaka huu ya UN ilisema kwamba tangu Oktoba 9 mwaka jana kulipoanza operesheni za jeshi la serikali dhidi ya Waislamu wa Rohingya, zaidi ya watu elfu 75 wamekimbilia nchini Bangladesh kutokana na mauaji na jinai wanazofanyiwa na wanajeshi wakishirikiana na mabudha wenye misimamo ya kuchupa mipaka.