IAEA yasisitiza kuwa Iran imefungamana na JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/world-i29974
Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA umetoa ripoti na kwa mara nyingine umethibitisha kuwa Iran imeheshimu kikamilifu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
(last modified 2025-06-15T08:05:10+00:00 )
Jun 03, 2017 07:51 UTC
  • IAEA yasisitiza kuwa Iran imefungamana na JCPOA

Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA umetoa ripoti na kwa mara nyingine umethibitisha kuwa Iran imeheshimu kikamilifu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Katika ripoti yake ya jana ambayo imesambazwa kwa nchi wanachama, IAEA imesema kufikia Mei 27, kiwango cha urutubishaji urani nchini Iran kilikuwa kilo 79.3, ikilinganishwa na kilo 300 ambazo Iran inaruhusiwa kuzalisha kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati yake na kundi la 5+1 linaloundwa na nchi za Russia, China, Ufaransa, Uingereza, Marekani pamoja na Ujerumani. 

Yukiya Amano, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA

Ripoti hii mpya ya IAEA ni ya pili tangu Rais wa Marekani, Donald Trump aingie madarakani ikizingatiwa kuwa ya kwanza ilitolewa mwezi Februari. 

Rais huyo wa Marekani anapinga makubaliano ya JCPOA yaliyofikiwa kati ya Iran na kundi la 5+1 mwaka 2015 na amekuwa akiyataja kama 'makubaliano mabaya zaidi duniani katika historia ya hivi karibuni.' Kadhalika aliahidi kuyachana katika siku yake ya kwanza ya kuingia Ikulu ya White House.

Rais Trump wa Marekani

IAEA imetangaza mara kadhaa kuwa Iran imetekeleza majukumu yake katika mapatano hayo ya nyuklia ambayo yalitiwa saini Julai mwaka 2015 na kuanza kutekelezwa Januari mwaka jana.