Ufilipino: Hatujaomba msaada wa Marekani kukabiliana na magaidi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i30352-ufilipino_hatujaomba_msaada_wa_marekani_kukabiliana_na_magaidi
Rais Rodrigo Duterte wa Ufilipino amesema nchi yake haijaomba msaada wa Marekani kwa ajili ya kupambana na genge la kigaidi lililoua wanajeshi 13 wa nchi hiyo Ijumaa iliyopita, kusini mwa nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 11, 2017 22:57 UTC
  • Ufilipino: Hatujaomba msaada wa Marekani kukabiliana na magaidi

Rais Rodrigo Duterte wa Ufilipino amesema nchi yake haijaomba msaada wa Marekani kwa ajili ya kupambana na genge la kigaidi lililoua wanajeshi 13 wa nchi hiyo Ijumaa iliyopita, kusini mwa nchi.

Duterte amenukuliwa na shirika la habari la Russia Today akiyasema hayo jana na kuongeza kuwa, madai ya kipropaganda yanayoenezwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa aliliomba jeshi la Marekani liende nchini humo kupamba na magaidi ni uvumi usio na msingi.

Rais wa Ufilipino amesema: "Binafsi sikuwa na habari yoyote na ghafla nikashtukia kikosi maalumu cha jeshi la Marekani kiko nchini eti kukabiliana na magaidi katika mji wa Marawi."

Kufuatia wanachama hao wa kigaidi kuudhibiti mji huo, jeshi la Ufilipino limetangaza marufuku ya kutotoka nje mjini humo.

Ndege ya kivita ya US kusini mwa Ufilipino

Kadhalika Rais Duterte hivi karibuni alisema kuwa, ili kumtia mbaroni Isnilon Hapilon, kiongozi wa kundi la kigaidi la Abu Sayyaf na kadhalika wapiganaji wa kundi la Maute kwa majina ya Abdullah na Omar ambao ni wafuasi wa genge la ukufurishaji la Daesh (ISIS), serikali yake itatoa kiasi cha dola elfu 40 kama zawadi kwa mtu atayefanikisha jambo hilo. 

Zaidi ya watu 200 wakiwemo watoto na wanawake wameripotiwa kuuawa hadi sasa na wanachama hao wa kigaidi. Wanajeshi 58 wa Ufilipino ni miongoni mwa watu waliouawa na magaidi hao tangu makabiliano kati ya pande mbili hizo yaanze Mei 23.