Korea Kusini: Pyongyang iwaachilie huru watu wetu na Wamarekani inaowashikilia
Waziri Mkuu wa Korea Kusini ameitaka serikali ya Korea Kaskazini kuwaalichilia huru raia wa nchi hiyo na wale wa Marekani ambao wanashikiliwa na serikali ya Pyongyang.
Lee Nak-yon ametoa ombi hilo baada ya kufariki dunia mwanafunzi mmoja raia wa Marekani aliyekuwa akishikiliwa katika jela za Korea Kaskazini. Ikumbukwe kuwa wakati Otto Warmbier mwanafunzi huyo wa Marekani alipoachiliwa huru kutoka katika jela huko Korea Kaskazini, alikuwa amepoteza fahamu.
Kitendo cha mwanafunzi huyo kupoteza maisha muda mfupi baada ya kuachiliwa huru na Pyongyang, kimeamsha hasira za jamii ya kimataifa ambazo zimeitaka Korea Kaskazini kuweka kando miradi yake ya nyuklia na kuheshimu haki za binaadamu. Otto Warmbier aliyezuiliwa nchini Korea Kaskazini kwa muda wa miezi 17, alifariki dunia baada ya kufikishwa Marekani. Hadi sasa raia sita wa Korea Kusini wanaendelea kushikiliwa katika jela za Korea Kaskazini kwa makosa tofauti. Tarehe 19 mwezi huu Rex W. Tillerson, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani aliiomba serikali ya Pyongyang kuwaachilia huru raia wengine watatu wa Marekani ambao wapo katika jela za nchi hiyo ya Asia. Katika hatua nyingine Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini ametoa mwaliko kwa Korea Kaskazini wa kushiriki katika michezo ya olimpiki itakayofanyika wakati wa msimu wa baridi kali mwaka 2018 katika mji wa PyeongChang, nchini Korea Kusini.
Rais Moon Jae-in ametoa mwaliko huo katika sherehe za ufunguzi wa mashindano ya taikondo (Taekwondo) ya ubingwa wa dunia mwaka 2017 ambayo yanafanyika katika mkoa wa Jeollabuk-do nchini Korea Kusini. Katika sherehe hizo rais huyo amesema kuwa, ikiwa wanamichezo wa Korea Kaskazini watashiriki michezo ya olimpiki mwaka 2018 itakuwa ni hatua kubwa ya kuboresha urafiki na usalama kati ya nchi hizo mbili.