Pyongyang: Trump anatekeleza siasa zile zile za Adolf Hitler wa Ujerumani
Serikali ya Korea Kaskazini imesema kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani anatekeleza siasa zile zile za Adolf Hitler, kiongozi wa zamani wa Kinazi nchini Ujerumani.
Korea Kaskazini imesema hayo Jumatatu ya leo kupitia shirika rasmi la habari la serikali katika wakati huu wa kukaribia safari ya Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini mjini Washington kwa ajili ya kukutana na Rais Donald Trump wa Marekani. Katika makala hayo, Pyongyang imesema kuwa, siasa za kupenda kujitanua za rais huyo wa Marekani ndizo siasa za Unazi wa karne 21 kwa kuwa hazitofautiani hata kidogo na zile zilizokuwa zinatekelezwa na Adolf Hitler.
Kwa mujibu wa rpoti hiyo, lengo na madhumuni ya Marekani ni kutaka kujikweza duniani kupitia njia ya kijeshi, suala ambalo halikubaliki. Kabla ya hapo pia, Korea Kaskazini ilimtaja Donald Trump kuwa mtu mwenye matatizo ya kiakili. Kadhalika Pyongyang imeiishutumu serikali ya Washington kwa kuizuilia Korea Kaskazini kupata vifaa vya tiba na kuitaja hatua hiyo kuwa ni kinyume na ubinaadamu na inakinzana na maadili. Imesema kuwa, hatua hiyo ni kama ile iliyochukuliwa na Adolf Hitler katika Vita vya Pili vya Dunia ambavyo vilisababisha zaidi ya watu milioni mbili kuuawa.
Katika safari yake mjini Washington Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini atakutana na kufanya mazungumzo na Donald Trump, ambapo ajenda kuu itakuwa ni juu ya kuhitimisha mipango ya silaha za nyuklia na makombora ya balestiki ya Korea Kaskazini. Kwa mara kadhaa serikali ya Pyongyang imekuwa ikisisitiza kuwa, vitisho vya Washington ndivyo vinavyochochea mgogoro katika Peninsula ya Korea.