Korea Kusini sasa yaomba mazungumzo na Korea Kaskazini
Huku mgogoro wa Peninsula ya Korea ukiendelea kutokota kufuatia vitisho vya Rais Donald Trump wa Marekani kwamba atatumia nguvu za kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini, Korea Kusini sasa imetaka mazungumzo yafanyike kutatua mgogoro uliopo.
Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini akizungumza mjini Hamburg Ujerumani alikokwenda kuhudhuria kikao cha nchi 20 tajiri kiviwanda duniani maarufu kama G20, amesema iwapo mazingira yatakuwa mazuri, basi yuko tayari kufanya mazungumzo wakati wowote ule na mahala popote pale na kiongozi wa Korea Kaskazini.
Amesisitiza kuwa, yamkini hii ikawa ni fursa ya mwisho kabisa ya mazungumzo na hivyo ni bora Korea Kaskazini ikubali kufanya mazungumzo na Korea Kusini.
Ombi la Rais wa Korea Kusini kwa Korea Kaskazini kuhusu kufanya mazungumzo ya kumaliza mgogoro wa Peninsula ya Korea ni jambo linaloonyesha kuwa, Moon Jae-in anaona kuna uwezekano wa kufanyika mazungumzo ya pande mbili baina ya Seoul na Pyongyang kuliko kuanzisha tena mazungumzo yaliyofeli ya pande sita ambayo mbali na Korea mbili, yalijumuisha pia Marekani, China, Japan na Russia. Mazungumzo ya Pande Sita ya Nyuklia ya Korea Kaskazini yalivunjika mwaka 2008 baada ya Marekani kukataa kutekeleza ahadi zake kwa Korea Kaskazini.
Tokea wakati huo hadi sasa, jitihada za kieneo na kimataifa za kuanza tena mazungumzo zimekuwa zikifeli kwa sababu Korea Kaskazini haiiamini tena Marekani. Aidha Pyongyang inasisitiza kuwa, mazungumzo hayo yataanza tu iwapo Marekani itaachana na sera zake za vitisho na uhasama na iache mazoezi yake ya kijeshi katika eneo hilo.
Ombi la Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini la kufanyika mazungumzo ya ana kwa ana baina ya Korea mbili limekuja baada ya Korea Kaskazini kufanya jaribio la kombora la balistiki la baina ya mabara hatua ambayo ilipelekea Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuitisha kikao cha dharura kujadili kadhia hiyo. Kufuatia jaribio hilo la kombora, Marekani imezidisha vitisho vyake dhidi ya Korea Kaskazini.
Nikki Haley, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa akizungumza kwenye kikao hicho cha Baraza la Usalama alisema majaribio ya makombora ya Korea Kaskazini ni jambo linaloondoa uwezekano wa utatuzi wa kidiplomasia wa mgogoro wa Rasi ya Korea na kwamba Marekani haitakuwa na njia nyingine ila kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Pyongyang.
Vitisho vya Marekani dhidi ya Korea Kaskazini ni jambo ambalo limepelekea Russia na China kuwa na wasiwasi mkubwa kwani nchi hizo mbili zinapinga vikali hatua yoyote ya kijeshi ya Marekani katika Rasi ya Korea.
Kwa hakika iwapo Marekani itatumia nguvu za kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini, basi itakuwa imevuka mstari mwekundu wa Russia na China, nchi ambazo zinasema hazitaruhusu kutokea vita katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Liu Jieyi, Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa amesema, chaguo la kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini halipaswi hata kutajwa.
Naibu Balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa Vladimir Safronkov pia alikuwa na msimamo sawa na huo ambapo amesema suluhisho la kijeshi katika mgogoro wa Korea Kaskazini linapaswa kuwekwa kando.
Ni kwa kuzingatia misimamo hiyo ya Russia na China ndio maana rais wa Korea Kusini akaonekana kujiweka mbali na misimamo ya kichochezi ya muitifaki wake mkuu yaani Marekani na kutaka mazungumzo yafanyike baina ya Pyongyang na Seoul.
Ametoa wito huo wa mazungumzo hasa kwa kuzingatia kuwa, katika kampeni zake za uchaguzi alitoa ahadi ya kubadilisha sera za kigeni za nchi yake hususan utatuzi wa mgogoro jirani yake wa kaskazini na ni sera na ahadi hizo ndio maana alishinda katika uchaguzi huo.
Ni wazi kuwa, iwapo Korea Kusini itaweza kufanya mazungumzo yenye manufaa na Korea Kaskazini, basi Marekani itakosa fursa ya kuzusha machafuko katika eneo hilo. Washington inazusha chokochoko katika katika fremu ya sera zake za kuvuruga usalama ili kufaidisha viwanda vyake vya kutengenza silaha, kwani ni kwa kueneza hofu tu ndipo itakapoweza kuziuzia Japan na Korea Kaskazini silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola.