Korea Kaskazini: Wabunge wa Korea Kusini waliotunyooshea kidole, watajuta
https://parstoday.ir/sw/news/world-i32130-korea_kaskazini_wabunge_wa_korea_kusini_waliotunyooshea_kidole_watajuta
Serikali ya Korea Kaskazini imewatahadharisha wabunge wa Korea Kusini kutokana na hatua yao ya kutoa taarifa ya kulaani majaribio ya hivi karibuni ya kombora yaliyofanywa na Pyongyang, na kusema kuwa, wabunge hao watajutia hatua hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 23, 2017 02:49 UTC
  • Korea Kaskazini: Wabunge wa Korea Kusini waliotunyooshea kidole, watajuta

Serikali ya Korea Kaskazini imewatahadharisha wabunge wa Korea Kusini kutokana na hatua yao ya kutoa taarifa ya kulaani majaribio ya hivi karibuni ya kombora yaliyofanywa na Pyongyang, na kusema kuwa, wabunge hao watajutia hatua hiyo.

Gazeti rasmi la serikali ya Korea Kaskazini la Rodong Sinmun limeandika: "Kile kilichofanywa na Bunge la Korea ya Kusini hakitakuwa na faida ghairi ya kuchochea ugomvi kati ya Korea mbili na hakitaimarisha umoja, maridhiano na mashirikiano kati ya Seoul na Pyongyang."

Bunge la Korea Kusini

Gazeti hilo limeongeza kuwa, hatua ya Bunge la Korea Kusini ya kujaribu kukwamisha juhudi za kujilinda serikali ya Pyongyang, lazima ipate jibu kali zaidi kutoka serikali ya Korea Kaskazini.

Itakumbukwa kuwa mwanzoni mwa wiki hii, Bunge la Korea Kusini liliitisha kikao na kulaani jaribio la kombora la balestiki la kuvuka mabara lililofanywa na Pyongyang hapo tarehe nne mwezi huu. Kadhalika gazeti hilo rasmi la serikali ya Korea Kaskazini la Rodong Sinmun limeandika kuwa, teknolojia ya kombora hilo la balestiki litapelekea kuimarishwa silaha za nyuklia za taifa hilo. Limeweka wazi zaidi kwamba, ikiwa Marekani itaendeleza siasa zake za uhasama dhidi ya Korea Kaskazini, basi Pyongyang nayo haitositisha miradi yake ya silaha za nyuklia.

Moja kati ya makombora hatari ya Korea Kaskazini

Limeandika tena kwamba, jeshi na raia wa Korea Kaskazini wameazimia kutetea taifa lao kwa kukabiliana na siasa za kupenda kujitanua za Washington. Katika hatua nyingine, serikali ya Korea Kusini imetangaza kuwa, uchumi wa Korea Kaskazini uliimarika mwaka jana 2016, licha ya nchi hiyo kuwekewa vikwazo mbalimbali na Umoja wa Mataifa.