Utawala wa Kifalme wa Saudi Arabia, susu la ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i32632-utawala_wa_kifalme_wa_saudi_arabia_susu_la_ugaidi
Ugaidi si jambo jipya duniani na wala halikuanza katika siku na miaka ya hivi karibuni. Hata hivyo inatupasa kusema kuwa, katika miaka ya hivi karibuni ugaidi umekuwa tishio kubwa na la kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 03, 2017 02:56 UTC
  • Utawala wa Kifalme wa Saudi Arabia, susu la ugaidi

Ugaidi si jambo jipya duniani na wala halikuanza katika siku na miaka ya hivi karibuni. Hata hivyo inatupasa kusema kuwa, katika miaka ya hivi karibuni ugaidi umekuwa tishio kubwa na la kimataifa.

Hii leo hakuna nchi inayoweza kudai kuwa, itasalimika na hatari ya ugaidi. Pamoja na hayo jambo linalooneka sasa kuhusu ugaidi ni tofauti ya tishio hilo kwa nchi mbalimbali. Hii ni kwa sababu, kwanza kabisa, baadhi ya nchi zinakabiliwa na tishio dogo zaidi la ugaidi zikilinganishwa na nyingine zinazokabiliwa na vitisho vikubwa na huenda vya kila siku. Pili ni kuwa, katika baadhi ya nchi magaidi wanafanya kazi kama watu binafsi na kupitia vitendo vya kujilipua kwa mabomu au kufanya mauaji ya kigaidi, na katika nchi nyingine kama Syria na Iraq ugaidi unafanywa na makundi kupitia vita na mapigano dhidi ya serikali za nchi hizo. 

Mauaji ya kutisha ya kundi la Daesh, Iraq na Syria

Hapana shaka kuwa, siasa za baadhi ya nchi zimekuwa na taathira kubwa katika kudhihiri na kupanuka makundi ya kigaidi. Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi hizo zilizokuwa na mchango mkubwa katika kuundwa na kupanuka makundi ya kigaidi katika eneo la Mashariki ya Kati, Afrika na kwengineko. Mwaka 2011 Saudi Arabia ilianza kutekeleza sera za kuiondoa madarakani serikali ya Syria na kuzuia mabadiliko ya mlingano wa nguvu kwa maslahi ya mrengo wa muqawama na mapambano dhidi ya Wazayuni na ubeberu kupitia njia ya kuyaunga mkono na kuyasaidia makundi ya kigaidi. Tunaweza kutaja makundi yanayojiita Ahraru Sham na Jaishul Islam kama mfano wa makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na kufadhiliwa na Saudi Arabia kwa shabaha ya kuiondoa madarakani serikali halali ya Syria. Ni kwa msingi huo huo pia ndiyo maana Saudi Arabia na Uturuki zimezuia kuwekwa makundi hayo mawili katika orodha ya makundi ya kigaidi. 

Makundi ya kigaidi yanayofadhiliwa na Saudia

Suala jingine muhimu ni kwamba, nchi kama Saudi Arabia mbali na kwamba zinayafadhili na kuyaunga mkono makundi ya kigaidi katika siasa zao za kigeni, vilevile muundo wa kijamii na kiutamaduni wa nchi hizo unatayarisha mazingira ya raia wao kujiunga na makundi ya kigaidi. Kwa mfano tu tunaweza kuashiria kuwa, watu 9 kati ya 15 waliotekeleza mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani walikuwa raia wa Saudi Arabia. Vilevile kiongozi wa zamani wa kundi la al Qaida, Usama bin Laden, alikuwa raia wa Saudi Arabia. Kwa sasa pia Hussein Sufan aliyeteuliwa kuwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Ahraru Sham ni raia wa Saudi Arabia na amehitimu katika Chuo Kikuu cha Mfalme Abdul Aziz nchini humo.

Hussein Sufan

Suala hili linaonesha kuwa, mfumo wa elimu wa Saudia ulioathiriwa na mafundisho ya Kiwahabi na kitakfiri, ni susu la kulea watu wenye mitazamo ya kigaidi na kikatili.

Pamoja na hali hiyo, jambo la kustaajabisha zaidi ni kuona utawala kama huo wa Saudia ukizituhumu nchi nyingine kuwa zinaunga mkono ugaidi na kudai kwamba, Riyadh inapambana na igaidi! Ukweli huo unaonekana katika mgogoro wa sasa wa Saudi Arabia na Qatar ambapo watawala wa Aal Saud wanadai kuwa, sababu ya mgogoro huo ni uungaji mkono wa Doha kwa makundi ya kigaidi!

Mwishoni inatupasa kusema kuwa, yumkini bali tuna yakini kwamba baadhi ya nchi za Kiarabu za Mashariki ya Kati zinayaunga mkono na kuyasaidia makundi ya kigaidi, lakini Saudi Arabia si tu kwamba inayaunga mkono na kuyasaidia makundi hayo ya kikatili, bali pia raia wa Saudia wenye fikra na itikadi za Kiwahabi na kitakfiri, ndio wanaoongoza makundi hayo ya kigaidi.