Korea Kaskazini: Chokochoko za Marekani zikiongezeka, tutaishambulia bila huruma
Kwa mara nyingine serikali ya Korea Kaskazini imetoa onyo kali kwa Marekani kwa kusema kuwa, ikiwa siasa za uhasama na kupenda kujitanua dhidi ya Pyongyang zitaendelea na hatimaye kuisukuma nchi hiyo kuingia katika vita vya nyuklia, basi Washington itakabiliwa na mashambulizi makali.
Taarifa iliyotolewa na serikali ya Korea Kaskazini imesema kuwa, ikiwa nchi hiyo itashambuliwa na Marekani, basi ardhi ya Marekani na kadhalika kisiwa cha Guam kilichopo magharibi mwa bahari ya Pasifiki chenye askari wa Marekani na zana nyingi za kijeshi na ndege za kivita, itakuwa katika shabaha ya makombora yake ya nyuklia. Indhari hiyo imetolewa ikiwa ni siku moja kabla ya kuanza maneva ya kijeshi kati ya Marekani na Korea Kusini. Maneva hayo yanatazamiwa kuanza Jumatatu ya kesho na kuendelea kwa muda wa siku 10 katika eneo la Korea.
Mgogoro kati ya Marekani na Korea Kaskazini umeendelea kushtadi katika eneo la Peninsula ya Korea. Hii ni katika hali ambayo hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulipasisha vikwazo mpya dhidi ya Korea Kaskazini. Kabla ya hapo pia Rais Donald Trump wa Marekani alitoa vitisho vikali kwamba, Pyongyang itashuhudia moto wa hasira ambazo hazijawahi kushuhudiwa na walimwengu, ambapo kufuatia matamshi hayo, Korea Kaskazini ilitangaza kuanza mpango wa kukishambulia kisiwa cha Guam ambacho ni mali ya Marekani.
Kufuatia tangazo hilo la Korea Kaskazini, wakazi wa kisiwa cha Guam walipatwa na wasiwasi mkubwa juu ya hatma yao. Gazeti la New York Times liliandika kuwa, tangu serikali ya Pyongyang ilipotangaza azma yake ya kutaka kukishambulia kisiwa hicho, wakazi wake wamepatwa na khofu kubwa, huku wengine wakilazimika kuondoka eneo hilo.