Trump; mchochezi wa ubaguzi wa rangi nchini Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i33752-trump_mchochezi_wa_ubaguzi_wa_rangi_nchini_marekani
Msimamo uliochukuliwa na rais wa Marekani, Donald Trump kuhusu machafuko ya hivi karibuni ya mjini Charlottesville huko Virginia na hatua yake ya kuwaunga mkono wabaguzi wa rangi walioshadidisha machafuko hayo unaendelea kulaaniwa na kulalamikiwa vikali ndani na hata nje ya Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 28, 2017 23:54 UTC
  • Trump; mchochezi wa ubaguzi wa rangi nchini Marekani

Msimamo uliochukuliwa na rais wa Marekani, Donald Trump kuhusu machafuko ya hivi karibuni ya mjini Charlottesville huko Virginia na hatua yake ya kuwaunga mkono wabaguzi wa rangi walioshadidisha machafuko hayo unaendelea kulaaniwa na kulalamikiwa vikali ndani na hata nje ya Marekani.

Mtandao wa habari wa The Hill umewaonya viongozi wa serikali ya Marekani ukiwaambia kwamba kutokea machafuko baina ya wabaguzi wa rangi na makundi ya kupinga ubaguzi wa rangi katika vyuo vikuu vya miji mbalimbali ya Marekani kwenye wiki zijazo ni jambo lisilozuilika tena.

Julian Zelizer, mwanahistoria na mtaalamu wa masuala ya kisiasa na kiutawala katika Chuo Kikuu cha Princeton amesema, malumbano na mashambulizi ya maneno ya rais wa Marekani Donald Trump na makundi mbalimbali ya nchi hiyo, yamezidi kuchochea machafuko, ukosefu wa amani na chuki za kibaguzi nchini Marekani.

Magenge ya wabaguzi wa rangi Marekani yakifanya machafuko

 

Kwa siku kadhaa sasa miji mbalimbali ya Marekani inashuhudia machafuko makubwa baina ya makundi yanayopinga ubaguzi wa rangi na yale yanayounga mkono ubaguzi huo, hususan baada ya Donald Trump kushindwa kuyalaani makundi ya wabaguzi wa rangi, bali kuyaunga mkono waziwazi na hata kusema kuwa, makundi ya wapinzani wa ubaguzi wa rangi nayo yana makosa katika machafuko hayo.

Msimamo huo wa Donald Trump umezusha mvurugano hata ndani ya serikali yenyewe ya Marekani ambapo Rex Tillerson, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo amekosoa matamshi ya kibaguzi ya Trump. Akizungumza na televisheni ya Fox News kuhusu matamshi ya kibaguzi yaliyotolewa na Donald Trump juu ya matukio ya Charlotteville, Tillerson amesema, Trump anazungumza kwa niaba yake mwenyewe na haliwakilishi kabisa taifa la Marekani. Kabla ya hapo pia Waziri  wa Mambo ya Nje wa Marekani alikuwa ametoa taarifa akilaani harakati za makundi ya kibaguzi nchini humo.