Aug 31, 2017 02:52 UTC
  • UN: Trump anachochea hujuma dhidi ya waandishi wa habari

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuwa, kitendo cha Rais Donald Trump wa Marekani cha kukejeli na kuvipaka matope vyombo vya habari huenda kikachochea hujuma dhidi ya waandishi wa habari.

Zeid Ra'ad al-Hussein alisema hayo jana Jumatano mjini Geneva na kuongeza kuwa, tabia hiyo ya Trump ya kukashifu vyombo vya habari vinavyoakisi na kufichua uozo na mapungufu katika serikali yake inaweza kuandaa mazingira ya kuchukiwa na hata kushambuliwa waandishi wa habari.

Amesema iwapo mwandishi yeyote wa habari atahujumiwa kutokana na matamshi ya kichochezi ya Trump dhidi ya vyombo vya habari, basi rais huyo awe tayari kubeba dhima ya shambulizi hilo.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kitendo cha Trump cha kuvikejeli na hata kutaja hadharani majina ya baadhi ya vyombo vya habari kama vile CNN, New York Times na Washington Post mbali na kuandaa uwanja wa kuhujumiwa waandishi wa habari wa mashirika hayo, ni hujuma ya moja kwa moja dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari.

Zeid Ra'ad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN

Ra'ad al-Hussein amesisitiza kuwa, kuvitukana vyombo vya habari na kudai kuwa taarifa au habari zao ni 'bandia' ni sumu ambayo taathira zake hasi zitashuhudiwa hivi karibuni iwapo mwenendo huo utaendelea.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni na taasisi ya Gallup yameonesha kuwa, kiwango cha kuchukiwa Donald Trump kinazidi kuongezeka nchini Marekani licha ya kupita miezi saba tu tangu kiongozi huyo ashike madaraka ya nchi. 

Kwa mujibu wa Gallup, zaidi ya theluthi mbili ya watu wanaompinga na kumchukia Trump wanasema ni kutokana na shakhsia yake mbaya na hasi.   

Tags