Korea Kaskazini: Japan inajitafutia matatizo kwa kushirikiana na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i33828-korea_kaskazini_japan_inajitafutia_matatizo_kwa_kushirikiana_na_marekani
Serikali ya Pyongyang imetoa tahadhari kwa Japan kwamba, nchi hiyo inajitafutia matatizo kutokana na hatua yake ya kushirikiana na Marekani na lengo lake la kutaka kusimika ngao ya makombora ya AEGIS nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 31, 2017 08:00 UTC
  • Korea Kaskazini: Japan inajitafutia matatizo kwa kushirikiana na Marekani

Serikali ya Pyongyang imetoa tahadhari kwa Japan kwamba, nchi hiyo inajitafutia matatizo kutokana na hatua yake ya kushirikiana na Marekani na lengo lake la kutaka kusimika ngao ya makombora ya AEGIS nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Korea Kaskazini kupitia shirika rasmi la habari la nchi hiyo imesema kuwa, kitendo cha Tokyo kusimama pamoja na Marekani ni sawa na kujiweka katika hatari ya kujiangamiza yenyewe hivi karibuni sana. Imesisitiza kuwa, hatua ya nchi hiyo kushirikiana na Washington dhidi ya Pyongyang imehatarisha usalama wake yenyewe.

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-Un

Aidha taarifa iliyotolewa na serikali ya Korea Kaskazini imesema kuwa mahusiano ya kijeshi ya nchi mbili yaani Japan na Marekani ni hatari kwa eneo zima la Korea na kwamba Tokyo haifahamu kuwa hatua hiyo inaitumbukiza katika kujiangamiza. Taarifa hiyo ya serikali ya Pyongyang imetolewa katika radiamali kufuatia mpango wa Tokyo wa kutaka kuinua kiwango cha mfumo wake wa makombora wa AEGIS. Kwa mujibu wa mpango huo, Japan inataka kusimika rada za kisasa kabisa za Marekani kwa ajili ya mfumo wake wa makombora ambao pia unaweza kuongezwa uwezo wake wakati wowote ule. Hatua ya Marekani kusimika ngao yake ya kisasa ya makombora nchini Korea Kusini na sasa nchini Japan imekuwa ikipingwa vikali na mataifa ya Russia, China na Korea kaskazini. Kwa mujibu wa mataifa hayo, usimikaji wa ngao hizo, utapelekea kukosekana mlingano katika eneo.