Desmond Tutu amtaka San Suu Kyi kukomesha mauaji ya Waislamu Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/world-i34105-desmond_tutu_amtaka_san_suu_kyi_kukomesha_mauaji_ya_waislamu_myanmar
Askofu Mkuu wa Afrika Kusini, Desmond Tutu amemtaka Mshauri Mkuu wa Serikali ya Myanmar na mshindi mwenzake wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Aung San Suu Kyi kukomesha mauaji yanayofanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 09, 2017 04:31 UTC
  • Desmond Tutu amtaka San Suu Kyi kukomesha mauaji ya Waislamu Myanmar

Askofu Mkuu wa Afrika Kusini, Desmond Tutu amemtaka Mshauri Mkuu wa Serikali ya Myanmar na mshindi mwenzake wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Aung San Suu Kyi kukomesha mauaji yanayofanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.

Tutu mwenye umri wa miaka 85 amesema hofu inayotawala Myanmar na mauaji ya kizazi yanayofanyika katika eneo la Rakhine vimemfanya ampashe waziwazi mtu ambaye alikuwa akimheshimu na kumtambua kuwa ni dada yake mpendwa na kumtaka aingilie kati na kusitisha mauaji hayo. Tutu amesema katika barua aliyomtumia Aung San Suu Kyi kupitia mtandao wa kijamii kwamba: "Mimi nimekula chumvi na sina tena uwezo kutokana na uzee na sasa nimestaafu rasmi, lakini nimeahidi nafsi yangu kwamba nitabakia kimya kuhusu masuala ya umma kutokana na huzuni kubwa niliyo nayo.

Desmond Tutu amemwambia San Suu Kyi kwamba: "Si laiki kwa mtu kama wewe kuongoza nchi ya Myanmar na kama gharama ya kupata vyeo vya juu vya kisiasa ni kunyamazia kimya mauaji ya Waislamu huko Rakhine basi gharama hiyo ni kubwa kupita kiasi".  

Image Caption

Wakati huo huo gazeti la Times la Uingereza limemshambulia vikali Mshauri Mkuu wa Serikali ya Myanmar, Aung San Suu Kyi kutokana na ukatili unaofanyika nchini humo dhidi ya Waislamu na kusema amepoteza sifa yake ya kimaadili. Limeandika kuwa baada ya kuwa kiongozi mkuu wa Myanmar, San Suu Kyi amekuwa mbaya kupita kiasi na kwamba mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel ni mshirika katika ukatili unaofanyika nchini humo.

Gazeti la Times limeitaka serikali ya Uingereza na washirika wake kumuwekea mashinikizo Kyi na kulaani mwenendo wake mbaya.

Vijiji vya Waislamu vinachomwa moto Myanmar

Taasisi mbalimbali za kimataifa pia zinasisitiza kuwa, Aung San Suu Kyi anapaswa kunyang'anywa Tuzo ya Amani ya Nobel kutokana na uhalifu na mauaji ya kimbari yanayofanyika nchini Myamnar dhidi ya Waislamu.