Antonio Guterres amtaka Suu Kyi azuie mauaji ya Waislamu wa Myanmar
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amemkosoa vikali Aung Suu Kyi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Myanmar na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel na kumtaka achukue hatua za kusitisha mauaji dhidi ya Waislamu wa Rohingya.
Antonio Guterres amemtaka Aung San Suu Kyi, kuchukua hatua za haraka kukomesha mateso na mauaji yanayofanywa dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa Myanmar.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, Aung Suu Kyi na serikali ya Mynamr wanapaswa kukomesha mara moja operesheni za jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa Rohingya.
Bwana Guterres ameongeza kuwa, kama Aung Suu Kyi hatachukua hatua itakayopelekea kusitishwa mauaji hayo, basi maafa ya kibinadamu katika nchi hiyo yatashadidi.
Aidha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa, Aung San Suu Kyi ambaye anatarajiwa kuhutubia taifa lake hapo Jumanne, ana kila nafasi ya kuingilia kati kuzuia maafa hayo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo maandamano ya kulaani jinai dhidi ya Waislamu wa Rohingya yameendelea kushuhudiwa kila pembe ya dunia, huku walimwengu wakimkosoa vikali Aung Suu Kyi, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel ambaye pia ni Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Myanmar kutokana na kutochukua hatua ya kuzuia mauaji hayo.
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, idadi ya Waislamu waliolazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na ukatili unaofanywa na serikali ya Myanmar hadi sasa imefikia laki nne.