Canada yatangaza kuwaunga mkono Waislamu wa Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/world-i34499-canada_yatangaza_kuwaunga_mkono_waislamu_wa_myanmar
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Canada ameeleza wasiwasi mkubwa alionao kuhusiana na hali mbaya wanayokabiliwa nayo Waislamu wa jamii ya Rohingya wa nchini Myanmar.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 18, 2017 03:43 UTC
  • Canada yatangaza kuwaunga mkono Waislamu wa Myanmar

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Canada ameeleza wasiwasi mkubwa alionao kuhusiana na hali mbaya wanayokabiliwa nayo Waislamu wa jamii ya Rohingya wa nchini Myanmar.

Bi Chrystia Freeland amesema kuwa, Justin Trudeau Waziri Mkuu wa Canada ametoa wito wa kuzingatia maafa na masaibu ya Waislamu wa Rohingya katika Mkutano wa mara hii wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).

Akihutubia jana katika mkusanyiko wa kuwaunga mkono Waislamu wa Rohingya katika mji wa Toronto, Bi Chrystia Freeland amesema kuwa, amezungumzia kadhia ya Waislamu wa Mynamr alipozungumza na Kofi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa na vile vile alipokutana na kufanya mazungumzo na mkuu wa sasa wa Kamisheni ya Uhakiki wa Mgogoro wa Myanmar.

Waislamu wa Kirohingya wakiwa katika maisha ya ukimbizi

Hayo yanajiri katika hali ambayo maandamano ya kulaani jinai dhidi ya Waislamu wa Rohingya yameendelea kushuhudiwa kila pembe ya dunia, huku walimwengu wakitaka kuchukuliwa hatua za haraka za kusitisha mauaji hayo.

Jana mji wa Toronto Canada ulishuhudia mkusanyiko mkubwa wa raia wa dini mbalimbali wakilaani mauaji dhidi ya Waislamu wa Rohingya na kutangaza himaya na uungaji mkono wao kwa Waislamu hao.

Hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa, idadi ya Waislamu waliolazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na ukatili unaofanywa na serikali ya Myanmar hadi sasa imefikia laki nne. Hadi sasa Waislamu elfu sita wa Rohingya wameuawa kikatili huko Myanmar na wengine elfu nane kujeruhiwa.