Kiongozi wa Myanmar atetea mauaji yanayotekelezwa dhidi ya Waslamu wa Rohingya
Kiongozi wa Myanmar hatimaye amevunja kimya chake kuhusiana na jinai na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaotekelezwa na magaidi wa Kibudha pamoja na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa Rohingya wanaoishi katika jimbo la Rakhine, ukiukaji ambao Umoja wa Mataifa umeutaja kuwa ni sawa na maangamizi ya kizazi dhidi ya Waislamu hao.
Aun San Suu Kyi, Mshauri Mkuu wa Serikali na ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Mynmar amevunja kimya chake kuhusiana na mauaji hayo ya kizazi ambayo yamepelekea maelfu ya Waislamu wa Rohingya kukimbilia katika nchi jirani ya Bangladesh, kwa kuyatetea bila kujali malalamiko ya kimataifa dhidi ya ukiukaji huo mkubwa wa haki za binadamu. Akihutubia taifa kwa mara ya kwanza leo Jumanne tokea kuanza kwa wimbi la pili la mauaji dhidi ya Waislamu hao wasio na hatia hapo tarehe 25 mwezi Agosti uliopita, Suu Kyi amekataa kulaani wala kukosoa wahusika wa jinai hiyo ambayo imehusisha kuchomwa vijiji, ubakaji, mauaji ya umati na kulazimishwa Waislamu wapatao 417, 000 kuhama ardhi zao katika jimbo la Rakhine.
Suu Kyi amekabiliwa na malamiko na ukosoaji mkubwa wa kimataifa kutokana na kimya chake kuhusu mauaji hayo ya kizazi yanayotekelezwa dhidi ya Waislamu wa Rohingya na Mabudha katili kwa ushirikiano wa jeshi la Mynmar, na hata wengi kumtaka mwanamke huyo asiye na huruma apokonywe tuzo ya amani ya Nobel aliyotunukiwa katika miaka ya huko nyuma. Katika machafuko hayo yanayowalenga Waislamu, nusu ya vijiji vya Waislamu wa Rohingya vimeteketezwa moto. Kiongozi huyo wa Myanmar awali alikanusha kuwepo kwa mauaji ya kizazi dhidi ya Waislamu hao katika jimbo la Rakhine akidai kuwa hiyo ni propaganda iliyokuwa ikienezwa kwa lengo la kuichafulia jina serikali yake. Kwa miongo kadhaa sasa, utawala wa Myanmar umekataa kutambua uraia wa Waislamu wapatao milioni 1.1 wa jamii hiyo ya Rohingya ukidai kuwa ni raia wa Bangladesh waliohamia nchini humo kinyume cha sheria. Waislamu hao walipokonywa uraia wa Myanmar mwaka 1982 na hivyo kunyimwa haki zote za kimsingi zikiwemo za kuabudu, kusafiri pamoja na huduma za elimu, chakula na tiba.