Kuhusu Waislamu wa Rohingya, Suu Kyi ni mdanganyifu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i34629-kuhusu_waislamu_wa_rohingya_suu_kyi_ni_mdanganyifu
Wakimbizi Waislamu wa kabila la Rohingya wanaoishi makambini nchini Bangladesh wamesema hotuba aliyotoa Aun San Suu Kyi Waziri wa Mambo ya Nje na ambaye pia ni Mshauri Mkuu wa Serikali ya Myanmar ni ya udanganyifu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 21, 2017 02:27 UTC
  • Kuhusu Waislamu wa Rohingya, Suu Kyi ni mdanganyifu

Wakimbizi Waislamu wa kabila la Rohingya wanaoishi makambini nchini Bangladesh wamesema hotuba aliyotoa Aun San Suu Kyi Waziri wa Mambo ya Nje na ambaye pia ni Mshauri Mkuu wa Serikali ya Myanmar ni ya udanganyifu.

Suu Kyi hatimaye amevunja kimya chake kuhusu maangamizi hayo ya kizazi wanayofanyiwa Waislamu wa Rohingya na serikali ya Myanmar na katika hatua ya kimaonyesho amebainisha kutiwa wasiwasi na ukiukaji wa haki za raia hao na kulaani suala hilo. Raia wanaoishi katika kambi ya wakimbizi wa Rohingya huko Bangladesh wameitaja hatua hiyo ya Suu Kyi kuwa ni ya udanganyifu na ya kuhadaa watu na kuitaka serikali ya Myanmar iziruhusu taasisi za kimataifa zilitembelee jimbo la Rakhine na kuandaa ripoti kuhusu jinai zinazofanywa na serikali ya nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa Rohingya. San Suu Kyi ameonyesha eti kuhuzunishwa na mauaji ya Waislamu wa Rohingya lengo likiwa ni kupunguza mashinikizo ya kimataifa dhidi yake sambamba na kufanyika vikao vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York. Hii ni kwa sababu Suu Kyi ambaye anajihesabu kuwa mtetezi wa haki za binadamu na mpigania ukombozi hivi sasa yuko chini ya mashinikizo makubwa ya ndani, kieneo na kimataifa kutokana na kukaa kimya na kutochukua hatua kuhusu maangamizi ya kizazi wanayofanyiwa Waislamu wa Rohingya huko Myanmar.

Aun San Suu Kyi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Myanmar na Mshauri Mkuu wa serikali 

Wakati huo huo taasisi za kimataifa zimemtaka Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Myanmar na Mshauri Mkuu wa Serikali ahitimishe jinai zinazofanywa na wanajeshi na Mabudha wenye misimamo mikali wa nchi hiyo. Hali hii ya mambo imemfanya Suu Kyi, ambaye wakati fulani alikuwa akiheshimiwa na wananchi wa Myanmar, atuhumiwe kuwa anashirikiana na watenda jinai dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.

William Hague, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Uingereza amenukuliwa na shirika la habari la ISNA akieleza kuwa: Hatua zinazotekelezwa dhidi ya Waislamu wa Rohingya huko Myanmar ni moja ya ukatili usio na kipimo wala mpaka dhidi ya jamii ya raia wa kawaida. Hakuna takwimu sahihi kuhusu watu waliouawa katika jimbo la Rakhine magharibi mwa Myanmar. Vijiji vinachomwa moto katika jimbo hilo huku kukijiri pia vitendo vya kinyama kama mauaji na ubakaji.

Vijiji vya Waislamu wa Rohingya vinachomwa moto 

Kulazimika Waislamu wa Rohingya kuzihama nyumba na makazi yao kumekuwa na maafa makubwa ya nyuma ya pazia kama kusambaratika familia, kushindwa watoto kusoma shule, kuongezeka njaa na umaskini, kuenea matatizo ya kiafya na kitiba pamoja na kujitokeza milipuko ya magonjwa mbalimbali; jambo litakalowasababishia matatizo ya kimwili na kiakili ya miaka mingi Waislamu hao wa Rohingya endapo  watarejea kwenye makazi yao. 

Likimnukuu Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, Shirika la Habari la Associated Press limearifu kuwa: Waislamu wa Rohingya ambao wamelazimika kuwa wakimbizi wanaugua maradhi ya kuambukiza na utapiamlo mkubwa. Suhula za matibabu zilizopo kwenye kambi za mipakani kwa ajili ya kuwatibu wakimbizi hazifai huku wakimbizi kadhaa wakiwa na majeraha ya risasi na kuhitajia kufanyiwa oparesheni. 

Kwa hali yoyote ile matamshi ya upotoshaji na ya kujaribu kuwahadaa walimwengu ya Aun San Suu Kyi kuhusu hali ya Waislamu wa Rohingya yanazidi kudhoofisha nafasi na hadhi yake huku jamii ya kimataifa ikimtaka mshauri huyo mkuu wa serikali ya Myanmar achukue hatua za kivitendo kukomesha maangamizi hayo makubwa ya kizazi yanayoendelea kushuhudiwa nchini humo.

Waislamu wanaonyongeshwa wa Rohingya wa nchini Myanmar