Waislamu Warohingya wanaendelea kuangamizwa kwa umati
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema ushahidi unaonyesha kuwa nyumba za Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar zinaendelea kuteketezwa katika jimbo la Rakhine.
Katika taarifa, Amnesty imesema taswira za satalaiti zinaonyesha moshi ukiwa umetanda katika vijiji vingi vya jimbo la Rakhine nchini Myanmar. Uteketezaji huo unatekelezwa na jeshi la Myanmar na Mabuddha wenye misimamo ya kufurutu ada.
Wakati huo huo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka jinai dhidi ya Waislamu wa Myanmar zisitishwe mara moja. Ameyasema hayo mjini New York katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu OIC. Araqchi aidha ametaja jinai zinazowakabili Waislamu wa Myanmar kuwa ni mauaji ya umati.
Wakati huo huo, Ofisi ya Uratibu ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Masuala ya Kibinaadamu (OCHA) Ijumaa ilitoa mwito wa kuongezwa bajeti ya misaada ya kibinaadamu kwa ajili ya wakimbizi Waislamu wa kabila la Rohingya waliokimbilia hifadhi katika nchi jirani ya Bangladesh. Taarifa hiyo imesema Waislamu takribani laki saba hivi sasa wametoroka Myanmar na kupata hifadhi huko Bangladesh.
Kwa miongo kadhaa sasa Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar wamekuwa wakishambuliwa na kuuawa kinyama na serikali ya Mabudha wa nchi hiyo ambapo askari wa serikali kwa kushirikiana na Mabudha magaidi wamekuwa wakitekeleza hujuma za kutisha dhidi ya watu hao kutokana tu na wao kuwa Waislamu. Kwa mujibu wa ripoti zilizotolewa hivi karibuni, zaidi ya Waislamu elfu sita wameuawa katika wimbi jipya la hujuma dhidi yao lililoanza tarehe 25 Agosti mwezi uliopita.