Venezuela: Marekani inafanya 'ugaidi wa kisaikolojia' dhidi yetu
Venezuela imesema Marekani inaendeleza kile ilichokitaja 'ugaidi wa kisaikolojia' dhidi ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini.
Akihutubu katika Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) hapo jana, Jorge Arreaza, Waziri wa Mambo ye Nje wa Venezuela amesema Washington inapanga njama ya kuisambaratisha nchi hiyo, huku akimtaja Rais Donald Trump wa Marekani kuwa mtu anayejifanya 'bepari wa dunia'.
Hii ni baada ya Washington kuijumuisha Venezuela katika orodha ya nchi nane ambazo raia wao wamepigwa marufuku kuingia Marekani.
Wiki iliyopita, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Venezuela alisema Trump ni mbaguzi na mtawala asiyetumia mantiki, baada ya rais huyo wa Marekani kuuambia mkutano wa UN mjini New York kuwa, atafanya kila awezalo kurejesha demokrasia nchini Venezuela.
Mwezi uliopita, Rais Nicolas Maduro wa Venezuela aliliagiza jeshi la nchi hiyo kufanya luteka ya nchi nzima ikiwa ni radiamali kwa vitisho vilivyotolewa hivi karibuni na Rais Donald Trump wa Marekani, aliyesema kuwa chaguo la kuishambulia kijeshi nchi hiyo lipo mezani.