Wamarekani milioni 50 wanaishi katika dimbwi la umasikini
Zaidi ya Wamarekani milioni 50 wanaishi katika dimbwi la umasikini huku kukishuhudiwa ongezeko la ukosefu wa ajira na kuzorota biashara nchini humo, uchunguzi mpya umebaini.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya Economic Innovation Group (EIG) yenye makao yake jijini Washington, mtu mmoja kati ya Wamarekani sita anaishi katika jamii zinazokumbwa na dhiki ambazo wengi wanaishi katika kiwango cha juu cha umasikini, pato duni na ukosefu wa elimu.
Uchunguzi huo unaonyesha kuwepo kiwango kikubwa cha ukosefu wa usawa wa kiuchumi pamoja na kuwa serikali ya Marekani inadai kuwa uchumi unafufuka. Taarifa hiyo ikiashiria pengo kubwa baina ya watu masikini na watu matajiri Marekani inasema jamii za matajiri zinashuhudia ustawi wa kasi kubwa huku maeneo ya watu masikini yakishuhudia udororoaji kiuchumi.
Taarifa hiyo pia inaonyesha ubaguzi mkubwa katika masuala ya kiuchumi Marekani kwani Wamarekani wenye asili ya Afrika na Wamarekani Asili (Wahindi Wekundu) ndio wanaoishi katika jamii zenye dhiki huku Wamarekani Wazungu wakiwa na hali bora kiuchumi.