Waislamu 14 wa Rohingya wafa maji baada ya boti yao kuzama
https://parstoday.ir/sw/news/world-i34967-waislamu_14_wa_rohingya_wafa_maji_baada_ya_boti_yao_kuzama
Kwa akali Waislamu 14 wa jamii ya Rohingya wamefariki dunia katika Mto Naf katika mpaka wa Myanmar na Bangladesh baada ya boti yao kuzama, wakikimbia mauaji na ukandamizaji unaofanywa na wanajeshi wa serikali ya nchi hiyo dhidi ya jamii hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 28, 2017 14:23 UTC
  • Waislamu 14 wa Rohingya wafa maji baada ya boti yao kuzama

Kwa akali Waislamu 14 wa jamii ya Rohingya wamefariki dunia katika Mto Naf katika mpaka wa Myanmar na Bangladesh baada ya boti yao kuzama, wakikimbia mauaji na ukandamizaji unaofanywa na wanajeshi wa serikali ya nchi hiyo dhidi ya jamii hiyo.

Polisi ya Bangladesh imethibitisha kutokeo mkasa huo na kusema watoto 10 na wanawake wanne wamefariki dunia katika ajali hiyo ya leo Alkhamisi.

Mohammad Sohel, muuza duka karibu na eneo la tukio ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, miili ya watu hao ilisombwa na mawimbi ya mto huo na kusukumwa ufukweni huku akitazama kwa mshangao.

Mapema mwezi huu, watoto 11 na wanawake 15 Waislamu wa Myanmar walifariki dunia katika tukio jingine la kuzama boti wakikimbilia usalama wao Bangladesh.

Hali ya kuogofya katika kambi za wakimbizi Bagladesh

Haya yanajiri huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likitahadharisha kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika kambi za wakimbizi huko Bangladesh unaotishia maisha ya Waislamu wa Rohingya wa Myanmar wapatao 436,000.

Kwa mujibu wa takwimu mpya za Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, idadi ya wakimbizi wa jamii ya Rohingya imepindukia laki 4 na elfu 80.