Uingereza yamtaka Trump aheshimu JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/world-i35509-uingereza_yamtaka_trump_aheshimu_jcpoa
Waziri Mkuu wa Uingereza amekariri kuwa London itaendelea kufungamana na kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya Iran, huku akimtaka Rais Donald Trump wa Marekani kuheshimu mapatano hayo ya kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 11, 2017 04:48 UTC
  • Uingereza yamtaka Trump aheshimu JCPOA

Waziri Mkuu wa Uingereza amekariri kuwa London itaendelea kufungamana na kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya Iran, huku akimtaka Rais Donald Trump wa Marekani kuheshimu mapatano hayo ya kimataifa.

Katika mazungumzo ya simu na Trump jana Jumanne, Theresa May amesisitiza kuwa makubaliano hayo yana umuhimu mkubwa kwa amani na usalama wa eneo.

Amesema kama tunavyomnukuu: "Kuna haja Washington isalie kwenye makubaliano hayo ya Vienna. Kutathminiwa kwa makini sambamba na kutekelezwa kwake ni jambo leye umuhimu mkubwa kwa usalama wa eneo hususan wakati huu."

Wakati huo huo, Boris Johnson, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: Nimefanya mazungumzo na mwenzangu wa Iran, Mohammad Javad Zarif na kumsisitizia kuwa Uingereza itazidi kufungamana na makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama JCPOA.

Theresa May na Trump wakisemezana jambo huko nyuma

Haya yanajiri siku moja baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) kwa mara nyingine tena kusisitiza kuwa Iran imeheshimu na kutekeleza majukumu yake kuhusu makubaliano ya nyuklia.

Licha ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Jim Mattis kuiambia kamati ya Seneti ya nchi hiyo hivi karibuni kuwa Washington haina chaguo jingine ghairi ya kubakia kwenye makubaliano ya nyuklia ya Iran na kujiondoa kwake kutakuwa na madhara makubwa kwa nchi hiyo, lakini Trump amekuwa akiyataja kama mapatano mabaya zaidi katika historia ya Marekani na kusisitiza kuwa Washington itajiondoa.