Ukosoaji mkali wa Venezuela dhidi ya Ulaya
Viongozi wa serikali ya Venezuela wamekosoa vikali juhudi za Umoja wa Ulaya na Marekani za kutaka kuufanya uchaguzi wa kieneo nchini humo kutokuwa na itibari.
Jorge Arreaza, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela amesema kupitia hotuba ya televisheni kuwa, baadhi ya serikali zinadhani kwamba zina haki ya kutambua au kutotambua asasi za kisheria za nchi nyingine. Viongozi wa Washington na vilevile wa Umoja wa Ulaya katika kukaribia kufanyika uchaguzi wa leo Oktoba 15 nchini Venezuela, wamefanya njama za kutilia shaka uchaguzi huo utakaoainisha mustakbali wa nchi hiyo.
Hatua hizo ni pamoja na vikwazo vya Marekani dhidi ya Venezuela na kwa mujibu wa ripoti kadhaa, Umoja wa Ulaya EU pia umekuwa ukifuata mkondo huo wa Washington katika kuiwekea vikwazo nchi hiyo. Uchaguzi wa Jumapili ya leo nchini venezuela unasimamiwa na waangalizi wa kimataifa na pia wataalamu wa masuala ya uchaguzi wanaoungwa mkono na mashirika ya kimataifa. Katika uchaguzi huo, magavana wa majimbo yote ya nchi hiyo isipokuwa lile la Caracas, ambao ni mji mkuu wa nchi hiyo, watachaguliwa. Caracas inaongozwa na serikali kuu ya Venezuela. Pamoja na hayo, baadhi ya wapinzani wa serikali ya Venezuela wamewataka wananchi kususia uchaguzi huo kiasi cha hata kutoa vitisho dhidi yao.
Kadhalika wapinzani wa serikali wanafanya njama za kuishawishi Marekani na Umoja wa Ulaya ziiingilie uchaguzi huo wa kieneo. Weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kwamba, uchaguzi wa leo utaainisha mustakbali wa taifa hilo, hasa ikitiliwa maananni kwamba, magavana ndio wanaosimamia shughuli za jeshi la polisi, hivyo ikiwa wapinzani watatwaa idadi kubwa ya magavana ni wazi kuwa maeneo yatakayokuwa chini ya magavana hao yatakuwa yametoka chini ya udhibiti wa serikali kuu ya Caracas. Pamoja na hayo, uchunguzi wa hivi karibuni unaonyesha kwamba licha ya wapinzani kuwa na wafuasi wengi mjini Caracas, lakini hawajaweza kuwavutia wakazi wa majimbo mengine. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Umoja wa Ulaya na Marekani zikatishia kutoutambua uchaguzi huo.
Alkhamisi iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitoa ripoti ya uingiliaji kwa kusema kuwa, raia wa Venezuela wana uwezo wa kupaza sauti zao nje ya masanduku ya kupigia kura. Katika kujibu matamshi hayo ya uingiliaji wa masuala ya ndani ya Venezuela, Bi Tibisay Lucena Mkuu wa Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi nchini humo (CNE) alisema: "Kila kitu kiko tayari kwa ajili ya ushiriki mkubwa wa wananchi katika uchaguzi na hakuna mtu aliye na uwezo wa kuzuia suala hilo. Raia wote wa Venezuela watatangaza maoni yao katika masanduku ya kupigia kura kwa namna ya amani." Mwisho wa kunukuu. Ripoti zinaonyesha kuwepo ushindani mkali kati ya waungaji mkono wa serikali na wapinzani katika uchaguzi huo wa leo.
Aidha wapinzani wamefanya kampeni kubwa kutokana na uungaji mkono wa kifedha na kisiasa wa Marekani na Umoja wa Ulaya. Kwa kutilia maanani suala hilo, wapinzani wanadai kwamba wameweza kupata wafuasi wengi katika miji mikubwa na kwamba serikali ina wafuasi katika miji midogo tu. Kiujumla ni kwamba matukio ya baadaye ya Venezuela, yatafahamika vyema baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa leo wa magavana majimboni. Hadi sasa uchaguzi wa hivi karibuni wa Baraza la Waasisi, ulionyesha kwamba raia wa nchi hiyo licha ya kuwepo mgogoro wa kiuchumi ndani ya taifa hilo, wanapinga aina yoyote ya utumiaji mabavu unaoenezwa na wapinzani wa serikali.