Guterres aonya juu ya kutumiwa vibaya mapambano dhidi ya ugaidi
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusu athari mbaya za sera za kupambana na ugaidi za baadhi ya nchi kwa suala la haki za binadamu.
Antonio Guterres ambaye alikuwa akihutubia wanachuo wa Kituo cha Utafiti wa Masuala ya Mashariki na Afrika nchini Uingereza amekosoa sera zinazotumiwa na baadhi ya nchi katika mapambano dhidi ya ugaidi na taathira zake mbaya kwa haki za binadamu na amevitaka vyombo vya habari vijiepushe kuelekeza kidole cha tuhuma kwa kaumu makhsusi kuhusiana na habari za matukio ya ugaidi.
Guterres amesema siasa za kupambana na ugaidi zisizoheshimu haki za binadamu yumkini zikapotoka njia na kuelekea kusiko.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye amejiepusha kutaja jina la nchi makhsusi amesema kuwa, makazi ya watu wengi wanaofanya mashambulizi ya kigaini ni nchi hizo hizo zinazokiuka haki za binadamu na suala hilo linachochewa zaidi ugaidi.
Amesisitiza kuwa, msingi wa ugaidi ni kuangamiza na kuharibu kabisa haki za binadamu kwa msingi huo mapambano dhidi ya ugaidi hayawezi kufanikiwa kupitia njia ya kuangamiza na kukiuka haki za binadamu.