Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar waendelea kufanyiwa ukatili
https://parstoday.ir/sw/news/world-i38563-waislamu_wa_jamii_ya_rohingya_nchini_myanmar_waendelea_kufanyiwa_ukatili
Ukatili na ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Myanmar unaendelea kuathiri maisha ya Waislamu wa kabila la Rohingya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 05, 2018 15:01 UTC
  • Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar waendelea kufanyiwa ukatili

Ukatili na ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Myanmar unaendelea kuathiri maisha ya Waislamu wa kabila la Rohingya.

Mwenyekiti wa tume huru ya kimataifa ya kusaka ukweli nchini Myanmar, FFMM, Marzuki Darusman amesema hayo alipozungumza na waandishi habari huko Geneva, Uswisi, baada ya timu yake kukutana na Warohingya huko Cox Bazar nchini Bangladesh ambako wamekimbilia kupata hifadhi na usalama wa roho zao.

''Hali haijatengamaa Myanmar kikamilifu. Tunaendelea kusikia uchomaji moto ukiendelea. Hili linaendelea kuathiri jamii hii.''

Amesema ukatili huo pia unajumuisha mauaji ya halaiki, ubakaji wa makundi na watu kukamatwa kiholela na kuongeza kuwa: ''Ushahidi huo kwa hakika utatumiwa kuandaa hitimisho na mapendekezo kwenye Baraza la Haki za Binadamu, yatakayojumuisha hatua za kinidhamu kwa wahusika wakuu wa ukatili huu wa halaiki."

Mwezi Disemba mwaka jana, wajumbe watatu wa tume ya FFMM, walitembelea Malaysia kwa siku tano na walikutana na jamii za wakimbizi wa jamii ya Rohingya. Ripoti yao itawasilishwa mbele ya Baraza la Haki la Umoja wa Mataifa mwezi Machi mwaka huu.

Kuanzia Agosti  25 mwaka huu hadi hivi sasa, vikosi vya usalama vya Myanmar vimechoma moto vijiji visivyopungua 350 katika eneo la Waislamu huko Rakhine, magharibi mwa nchi hiyo.

Wakimbizi Waislamu Warohingya wakikimbia makazi yao ya jadi yanayoteketezwa kwa moto na jeshi la Myanmar

Katika makubaliano yaliyofikiwa baina ya Aung San Suu Kyi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Myanmar na Abul Hassan Mahmud Ali, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Bangladesh, serikali ya Myanmar iliahidi kuwarejesha nyumbani wakimbizi wa Kiislamu wa nchi hiyo ambao filihali wanaishi katika mazingira magumu sana kwenye katika mpaka wa nchi mbili hizo.

Jinai za jeshi la Myanmar na Mabudha wa nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya zinaendelea katika hali ambayo, serikali ya nchi hiyo iliahidi kuandaa mazingira ya kurejea makwao wakimbizi wa Kirohingya.