Erdogan: Uturuki imechoka kusubiri kujumuishwa EU
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema Waturuki wamechoka kusubiri kujua iwapo nchi yao itajumuishwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya au la.
Rais Erdogan aliyasema hayo jana Ijumaa katika kikao na waandishi wa habari pamoja na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa mjini Paris na kubainisha kuwa, EU itambue kuwa Uturuki haitasubiri daima kujua hatima ya uanachama wake kwenye umoja huo.
Erdogan amesema wakati umefika kwa umoja huo kutoa uamuzi wa iwapo Uturuki itajiunga na EU au la na kwamba taifa hilo limechoka na mzaha na karata ya umoja huo.
Amesema subira ya Waturuki inaelekea ukingoni na wakati umefika kwa EU kuamua iwapo ina nia ya kweli ya kutaka Uturuki ijiunge nayo au la.
Itakumbukwa kuwa, nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Ulaya ilianzisha jitihada za kujiunga na EU miaka ya 60 na kutuma ombi rasmi la kujiunga na umoja huo mwaka 1987.
Hata hivyo mazungumzo rasmi ya kujadili uwezekano wa Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya yalianza mwaka 2005, na miaka 12 baadaye, nchi hiyo imeachwa katika njia panda.