HRW: Marekani, Uingereza na Ufaransa zisitishe kuiuzia silaha Saudi Arabia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i38669-hrw_marekani_uingereza_na_ufaransa_zisitishe_kuiuzia_silaha_saudi_arabia
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch amezitaka Marekani, Uingereza na Ufaransa ziache kuiuzia silaha Saudi Arabia.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Jan 08, 2018 04:32 UTC
  • HRW: Marekani, Uingereza na Ufaransa zisitishe kuiuzia silaha Saudi Arabia

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch amezitaka Marekani, Uingereza na Ufaransa ziache kuiuzia silaha Saudi Arabia.

Kenneth Roth ameandika katika ukurasa wake wa twitter kuwa wakati umefika sasa kwa Marekani, Uingereza na Ufaransa kuacha kuiuzia silaha Saudia. Amesema kuwa silaha hizo zinatumiwa kuipiga Yemen na kuwasababishia njaa raia wa nchi hiyo wasio na hatia. 

Wanachama 250 wa taasisi moja mashuhuri ya kimataifa inayohusika na masuala ya kisiasa, kiutamaduni na kielimu hivi karibuni waliwaandikia barua Rais Donald Trump wa Marekani, Emmanuel Macron wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Uingereza Bi Theresa May, nchi kubwa tatu zinazoidhaminia Saudia silaha katika vita huko Yemen wakisisitiza kuwa ni siku elfu moja sasa ambapo Yemen inakabiliwa na vita ambavyo vimevuka mpaka na kuwa maafa mabaya zaidi ya kibinadamu kuwahi kushuhudiwa leo hii duniani. 

Kuenea kipindupindu ni moja ya masaibu yanayoikabili Yemen kutokana na vita vilivyoanzishwa na Saudia 

Barua hiyo iliyoandikwa chini ya anwani "siku elfu moja za vita", "Yemen haina tena subira" ambayo imechapishwa katika gazeti la Lemonde la Ufaransa imewataka viongozi wa nchi hizo tatu kuhitimisha uungaji mkono wao wa silaha kwa utawala wa Saudi Arabia. Saudia huku ikungwa mkono na Marekani, Ufaransa na Uingereza ilianzisha uvamizi wa kijeshi katika nchi ya Kiarabu ya Yemen mwezi Machi mwaka 2015 na kisha kuizingira nchi hiyo baharini, nchi kavu na angani.