Mwanaharakati Pakistan: Dini ya Uislamu haihusiki hata kidogo katika kumwaga damu
Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kisiasa na Kidini nchini Pakistan, amesema kuwa Uislamu wa kweli hauhusiki kwa namna yoyote na umwagaji damu unaofanywa na makundi ya kigaidi.
Muhammad Abdul-Basit ameyasema hayo katika kongamano lililopewa jina la 'Nafasi ya Kiroho ya Maulama katika Kukabiliana na Wimbi la Ugaidi' ambapo sambamba na kukosoa utambulisho wa nchi za Magharibi juu ya ugaidi amesema kuwa, Wamagharibi wanatakiwa kuutenga mbali ugaidi na dini tukufu ya Kiislamu. Amesisitiza kwamba, Uislamu wa kweli hauwezi kuwa na mahusiano yoyote na ugaidi.
Kadhalika Abdul Basit amekosoa vikali fikra yoyote ya kuitenga mbali dini ya Uislamu na siasa na kuongeza kuwa, Uislamu ni mfumo kamili wa utawala unaotegemea misingi ya uadilifu na kuheshimu itikadi na mtazamo wa mwingine. Katika kongamano hilo, Shahabud-Din Darai, mratibu wa kituo cha utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Pakistan amesema kuwa, Uislamu ni dini ya amani na kuoneana huruma, maridhiano na udugu na kwamba kuna haja ya kuandaliwa uwanja kwa ajili ya kuiarifisha sura halisi ya dini hii duniani ili watu waweze kuyafahamu mafundisho yake ya kuvutia.